Serikali yatoa maelekezo muhimu kwa watumishi wote wa umma

NA JAMES K.MWANAMYOTO

KAIMU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amewaasa Watumishi wa Umma nchini kuacha tabia ya kutowathamini wananchi wa kawaida wanaofuata huduma katika Taasisi za Umma kwani mishahara wanayolipwa inatokana na kodi za wananchi hao, hivyo wanastahili kuthaminiwa na kupewa huduma bora.
Sehemu ya Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier (hayupo pichani) alipokuwa akifunga kikao kazi cha watumishi hao jijini Dodoma kilicholenga kutatua changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake.

Bw. Xavier Daudi ametoa nasaha hizo jijini Dodoma, wakati akifunga Kikao kazi cha siku mbili kilichoandaliwa na ofisi yake na kuhudhuriwa na Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi wa Halmashauri za Wilaya 35 nchini.

Bw. Daudi amesema, kumekuwa na tabia ya kutowathamini wananchi wa kawaida wanaofuata huduma katika Taasisi za Umma. Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akizungumza na Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha maafisa hao kutoka Halmashauri za Wilaya 35 za Tanzania kilichoandaliwa na ofisi yake kwa lengo la kutatua changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuzi zake. 

“Posho za kujikimu na nauli mlizolipwa ili kuhudhuria kikao kazi hiki zinatokana na kodi za wananchi wa kawaida na ndio maana Serikali inawatambua kama wadau namba moja, hivyo hatuna budi kuwathamini na kuwapatia huduma bora kwa mujibu wa Mikataba ya Huduma kwa Mteja ya taasisi zenu,” Bw. Daudi amefafanua.

Ameongeza kuwa, wananchi wana matarajio makubwa ya kupata huduma bora katika Taasisi za Umma na ndio maana Serikali ilitekeleza Programu za Mabadiliko katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kukidhi matarajio ya wananchi.

Kutokana na matarajio hayo ya wananchi, Bw. Daudi amewataka watumishi kwa nafasi zao, pindi wanapotoa huduma kuzingatia mazingira na mahitaji ya wananchi ikiwa ni pamoja Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Hilda Kabissa akieleza lengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuandaa kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria jijini Dodoma kabla ya kikao kazi hicho kufungwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi. 

“Kama tusipoifahamu vizuri Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake pamoja na mazingira na mahitaji halisi ya wananchi na watumishi wenzetu tunaowahudumia, huduma zetu haziwezi kukidhi matarajio yao na yataibuka malalamiko dhidi ya huduma zinatolewa na taasisi za Serikali,” Bw. Daudi amesisitiza.

Bw. Daudi ameainisha kuwa, katika maeneo mengi ya kazi kuna malalamiko mengi sana lakini ni kwasababu katika utendaji kazi wa kila siku baadhi ya watumishi hawazingatii Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.
Mwenyekiti wa kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria, Bw. Maganiko Msabi akitoa neno la shukrani kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi mara baada ya Kaimu Katibu Mkuu huyo kufungua kikao kazi cha Maafisa hao jijini Dodoma.

Bw. Daudi ametoa rai kwa watumishi wasio waadilifu kubadilika kwani wananchi hivisasa wana ufahamu mkubwa wa haki zao hasa katika kupata huduma bora.

Washiriki wa kikao kazi hicho cha siku mbili, wamepata fursa ya kujengewa uwezo kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake, Maadili na Ushughulikiaji wa Malalamiko katika Utumishi wa Umma, Ushughulikiaji wa Masuala ya Kinidhamu na Ushughulikiaji wa Mafao kwa Watumishi wa Umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news