Wanaotoka kaya maskini kujengewa mabweni mkoani Simiyu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Simiyu,Mheshimiwa David Kafulila amesema kuwa, watoto wanaoishi katika kaya ambazo zipo kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) watajengewa mabweni kwa ajili ya kuwasaidia kupata uhakika wa eneo la kulala, kula mchana, usiku na waweze kusoma ili waje kubadilisha maisha yao na familia zao kwa ujumla. 
Amesema mkoa una jumla ya watoto 60,000 wa shule za msingi na 10,000 wa shule za sekondari na wote wanatoka kaya maskini zilizopo kwenye mpango huo huku akiongeza kuwa kuna mpango wa kujenga mabweni katika Shule ya Matongo na tayari ameshazungumza na watu wanaojenga mradi wa reli ya kisasa (SGR) ili kuwasaidia wanafunzi hao.

“Nimezungumza na watu wa SGR wanaojenga reli ya kisasa, tumekubaliana kwamba watajenga mabweni sita kwa mwaka huu na yatakuwa kwa ajili ya watoto wanaotoka kaya maskini ambazo zipo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini ( TASAF ) ili badala ya kurudi nyumbani wakitoka shule waende kwenye mabweni ambapo wanapata uhakika wa kula mchana,”amesema Kafulila. 

Aidha, Kafulila amesema tayari wamekubaliana kujenga na kukarabati majengo yaliyopo Shule ya Matongo ambayo ilijengwa kabla ya kuanzishwa kwa mkoa wa Simiyu (ilianzishwa bado ikiwa mkoa wa Shinyanga) na ilikuwa haitumuki huku akiongeza kuwa lengo ni kuwasaidia watoto wa kike. 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange amesema, shule hiyo iliyopo Matongo ilijengwa kabla ya kuanzishwa kwa mkoa wa Simiyu hivyo wanakwenda kuihuisha shule hiyo ili iweze kutumika kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanaotoka kwenye kaya maskini zilizopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) sambamba na watoto yatima lengo likiwa wapate . 

“Maono ya mkuu wetu wa mkoa na ya wilaya ni kuona wanafanikisha kile kilichokusudiwa na viongozi waliokuwepo kipindi hicho cha kuanzisha wazo la ujenzi wa shule hiyo ambayo awali ilijengwa kwaajili ya wasichana pia,"amesema Kapange .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news