Waziri Mhagama atoa onyo kwa maafisa sheria na utumishi

NA JAMES K.MWANAMYOTO 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amekemea tabia ya Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi Serikalini kukwepa jukumu lao la kuwapa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi watumishi wanaowasimamia na badala yake huwashauri kuandika barua kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili kupewa ufafanuzi wa masuala yao ya kiutumishi.
Sehemu ya Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha watumishi hao jijini Dodoma kilicholenga kutatua changamoto katika utekelezaji wa sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake.

Mhe. Jenista amesema, barua nyingi za kuomba ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi zinazowasilishwa ofisini kwake zinatoka kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri wakati Serikali imeajiri Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi katika Halmashauri zote nchini ili kufanya kazi hiyo. 

“Badala ya nyie Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa watumishi mnaowasimamia, mnawahamasisha waandike barua kwenye ofisi yangu kupata ufafunuzi, jambo ambalo si sahihi na halikubaliki,” Mhe. Jenista amefafanua. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria kutoka Halmashauri za Wilaya 35 za Tanzania (hawapo pichani) jijini Dodoma. 

Ameongeza kuwa, Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi Serikalini wanatakiwa kutumia nyadhifa zao kuwashauri Viongozi wao kuwahudumia watumishi ipasavyo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na maelekezo yanayotolewa na Serikali.

Mhe. Jenista amehoji uwepo wa Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi katika nafasi zao ikiwa wanashindwa kutatua changamoto za kiutumishi zinazowakabili watumishi wanaowasimamia ambazo ziko ndani ya uwezo wao.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria jijini Dodoma. 

“Afisa Sheria au Afisa Utumishi wa Halmashauri unajisikiaje watumishi katika kituo chako cha kazi kusafiri umbali mrefu kwa lengo la kuwasilisha masuala yao kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI ili yaweze kufanyiwa kazi wakati na wewe upo na masuala hayo yapo ndani ya uwezo wako kiutendaji,” Mhe. Jenista amehoji. 

Mhe. Jenista amesema kuwa, kuna barua nyingine ukisoma na kufanya uchambuzi unabaini kuwa mtumishi ameonewa na mwajiri wake na mwajiri huyo huyo anamshauri mtumishi huyo kuwasilisha suala lake Ofisi ya Rais Utumishi badala ya kulitatua. 
Mwenyekiti wa kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria, Bw. Maganiko Msabi akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya Mhe. Jenista kufungua kikao kazi cha Maafisa hao jijini Dodoma.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri kufungua kikao kazi hicho, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema, ofisi yake imeandaa kikao kazi hicho kwa lengo la kutatua changamoto ya baadhi ya Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi kutozingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika utendaji kazi wao. 

Bw. Daudi amesema Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi wana jukumu kubwa la kuhakikisha Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo inafuatwa ili kutenda haki katika utoaji wa huduma bora kwa umma. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria mara baada ya kufungua kikao kazi cha watumishi hao jijini Dodoma.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimeandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kinahudhuriwa na Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi wa Halmashauri za Wilaya 35 nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news