Waziri Profesa Mkenda:DIT tengenezeni vipuri vya vyombo vya moto

NA MWANDISHI MAALUM, WyEST 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kujitanua zaidi kwa kutengeneza vipuri vya vyombo vya moto ikiwemo vya bajaji na pikipiki.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo. 

Ameyasema hayo Januari 28, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea taasisi hiyo ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa hapo ambapo amesema tunaweza kukua kiteknolojia kwa kuboresha vitu ambavyo tayari vimeshatengenezwa na nchi nyingine. 

“Nimefurahi sana kuona mna kampuni inayosaidia kubiasharisha bidhaa za ubunifu ila niwatake mboreshe kwa kutengeneza vipuri ambavyo vinahitajika sana kama vya bajaji na pikipiki,”amesema Prof. Mkenda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (mwenye tai) akiwa ameongozana na Mkuu wa Taasisi ya DIT, Prof. Preksedis Ndomba (kushoto) na maafisa wengine kutoka Wizarani na DIT, wakati Waziri huyo alipotembelea taasisi hiyo. 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akipewa maelekezo na Dkt. Christian Budoya kuhusu mfumo wa kuangalia na kutawala magonjwa ya mlipuko Ukanda wa Afrika Mashariki wakati alipotembelea taasisi ya DIT.

Aidha, Waziri Mkenda ameipongeza taasisi hiyo kwa kuwa na kampuni inayosaidia kubiasharisha bunifu mbalimbali na kuwataka DIT kuhamisha ujuzi wa kiteknolojia kutoka nchi nyingine na kuja kuutumia hapa nchini katika uzalishaji wa bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya jamii. 

“Tunaweza tukaleta nchini kitu ambacho kimezalishwa mfano nchi ya Uturuki kisha tukaangalia uwezekano wa kukitengeneza na kukiuza ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wetu,” amesema Prof. Mkenda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Wizarani na Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo.

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda ameusisitiza uongozi wa DIT kuendelea kujenga na kukuza ushirikiano na taasisi nyingine hasa za nje ya nchi ili kubadilishana wataalamu watakaosaidia kuendelea kukuza teknolojia nchini. 

Kwa upande wake Mkuu wa taasisi hiyo, Prof. Preksedis Ndomba amesema wamepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji wa taasisi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news