Wizara ya Ardhi yaja na ufumbuzi mwingine katika utatuzi wa kero za ardhi nchini

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja kwa lengo la kuondoa kero za wananchi katika masuala ya ardhi.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akifuatilia upokeaji malalamiko ya wananchi kwenye kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi mara baada ya kukizindua leo Januari 7,2022 jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo. 

Uzinduzi wa kituo hicho umefanywa leo Januari 7,2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Waziri Lukuvi alisema, kwa kutumia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na habari yaliyopo sasa wizara yake imeona zipo baadhi ya huduma za ardhi zinazoweza kutolewa kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii ambazo hazimlazimu mwananchi kufika ofisi za ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizindua Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi leo Januari 7, 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Mary Makondo. 

‘’Wizara imeanzisha kituo cha Mawasiliano kwa Wateja kitakachotoa huduma ya mawasiliano moja kwa moja na mwananchi kwa kutumia simu na ujumbe wa maneno kupitia Whatsup ambapo majibu au ufafanuzi utatolewa kwa wananchi na wataalamu wa ardhi,"amesema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, Kituo hicho cha Mawasiliano kwa Wateja kina wataalamu wabobezi katika masuala ya ardhi waliopata mafunzo yakinifu ya kuifanya kazi ya kutoa huduma kwa wateja kwa weledi na kutoa majibu kwa wakati.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi David Malisa kuhusiana na namna ya Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi kinavyopokea malalamiko ya Wateja alipokizindua leo Januari 7, 2022 jijini Dodoma. 

Aidha, Waziri Lukuvi alitumia fursa ya uzinduzi wa kituo hicho kuwataka wananchi kukitumia kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi kuwasilisha kero mbalimbali zikiwemo za matapeli wa ardhi, watumishi wa sekta ya ardhi wasio waaminifu pamoja na wale madalali wanaochukua fedha za wapangaji na kusisitiza kuwa, anayepaswa kutoa fedha kwa madalali ni mwenye nyumba na siyo mpangaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia ndege ya kuchukua picha za anga (Drones) kwa ajili ya uandaaji ramani za msingi za upimaji leo Januari 7, 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Mary Makondo.

Ameongeza kwa kusema kuwa, kupitia kituo hicho mwananchi atalazimika kupiga simu na kuongea moja kwa moja na watoa huduma kupitia namba 0739-646-885 au kutuma ujumbe wa maneno kupitia mtandao wa WhatsApp kwa namba hizo. Kituo hicho kitakuwa wazi siku za kazi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

‘’Ni matumaini yangu kituo hiki kitatoa fursa kwa wananchi kupata huduma za ardhi kwa haraka, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu kwa kuwa mwananchi hatakazimika kufika ofisi za ardhi endapo huduma anayohitaji anaweza kuipata kupitia simu,"amesema.

Ametoa rai kwa wananchi kukitumia kituo hicho kwa kupiga simu na kutuma ujumbe wa maneno kupitia namba ya simu iliyotangazwa na kutumia tovuti ya wizara kupata huduma kwa urahisi bila usumbufu ili kuepuka gharama za kusafiri sambamba na kutumia muda mwingi kufuata huduma hizo ofisi za wizara makao makuu, ofisi za ardhi za mikoa na halmashauri.

Uanzishwaji wa Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja ni moja ya mikakati mbalimbali ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisdha huduma kwa wateja wa ardhi zinaboreshwa na zinatolewa kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Post a Comment

0 Comments