CCM yavuna 150 kutoka CUF,CHADEMA mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

WANACHAMA 150 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Wilaya ya Bunda, Serengeti na Musoma mkoani Mara wamevihama vyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. 
Wanachama hao wamejiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi leo Februari 10 2022, Makao makuu ya CCM Mkoa wa Mara yaliyopo Mjini Musoma baada ya kukabidhi kadi za vyama vyao kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Samwelly Kiboye katika hafla fupi ya kuwashukuru wanachama wa chama hicho na viongzozi wote walioshiriki kufanikisha sherehe za kitaifa za kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi zilizofanyika Kitaifa Mjini Musoma Februari 5, 2022. 

Maimuna Hassan Matola kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambaye aligombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kushika nafasi ya nne, amesema kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na Rais Samia zimemfanya achukue uamuzi wa kujiunga na CCM kwani ndicho chama pekee chenye dira na uwezo thabiti wa kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania. 
Amesema kuwa, katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia miradi mbalimbali ya kimkakati imeendelea kufanywa kikamilifu ikiwemo ujenzi wa miradi ya maji, afya, barabara, madaraja vyumba vya madarasa pamoja na utafutaji wa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi jambo ambalo linapaswa kupongezwa na Watanzania wote.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wanachama hao Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Samwelly Kiboye (Namba Tatu) amewataka wana CCM mkoani humo kutowabeza wanachama wa vyama vya upinzani wanaojiunga na Chama Cha Mpinduzi, bali wawape ushirikiano na kuzidi kukijenga chama kwa pamoja. 
Kiboye amesema, hakika kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya chama hicho chini ya Rais Samia Hassan zimeendelea kulifanya taifa kusonga mbele kimaendeleo na kwamba kila mwananchi anawajibu wa kuunga mkono juhudi hizo. 

Aidha, amewahimiza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi katika wilaya za mkoa huo, kufuatilia kwa Karibu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao iweze kuendana na thamani ya fedha zinazotolewa na serikali. 
Kiboye, amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Mara na wanachama wa CCM kwa umoja na mshikamano waliounesha katika sherehe za kuzaliwa kwa CCM ambazo zilifanyika Mjini Musoma na kusema kuwa, wakishiriki vyema ikiwemo kudumisha amani na usalama kipindi chote cha maandalizi hadi kutamatisha.

Post a Comment

0 Comments