Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) yatenga milioni 859/- ujenzi chujio la kutibu maji

NA SOPHIA FUNDI

MAMLAKA ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) mkoani Arusha imetenga kiasi shilingi milioni 859,150,000 katika ujenzi wa mradi wa chujio la kutibu maji karibu na lango la Loduare maarufu mto mama Hhau.
Akizungumza na wanahabari leo Februari 10,2022 Naibu Kamishna wa Huduma za shirika hilo, Needpeace Wambuya amesema kuwa, ujenzi wa mradi huo unatumia teknolojia ya kisasa ambayo itaruhusu kiwango cha lita milioni 1.5 kutibiwa kwa siku ambacho kitatosheleza mahitaji ya walengwa.

Amesema kuwa, mradi huo unajengwa ili kuboresha ubora wa maji yanayotumiwa na watalii katika lango la Loduare,hoteli za kitalii zilizoko maeneo ya jirani,makao makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,Hospitali ya Kilutheri Karatu na baadhi ya wananchi wa eneo la Njiapanda wilayani Karatu kuwa katika viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Huduma za Jamii, Daniel Chegere amesema kuwa, mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2021mwezi Julai na utakamilika mwaka 2022 Juni 30.
Anesema kuwa, mradi huo umegawanyika katika awamu mbili ambapo tayari imetumika shilingi milioni 309,470,840 ikiwa ni asilimia 80 ya mradi kukamilika.

Naye Mhandisi Godlove Sengele ametaja changamoto mbalimbali zinazowakabili wakati wa ujenzi kuwa ni pamoja na kuadimika kwa saruji na ukosefu wa baadhi ya vifaa vya ujenzi katika soko.

Amesema kuwa wanufaika wa mradi huo watarajie maji kuwa kwenye ubora wa WHO na TBS kwani yakitoka kwenye chanzo kwa maana ya mtoni yatapitia kwenye chujio hilo ambalo limejengwa kwa teknolojia inayokubalika kitaifa na kimataifa.

Post a Comment

0 Comments