'Mfalme Zumaridi' mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za usafirishaji haramu wa binadamu, unyonyaji

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Diana Edward Bundala maarufu Mfalme Zumaridi (39) kwa tuhuma za usafirishaji haramu wa binadamu zaidi ya 140 na unyonyaji.
Pia jeshi hilo limewaachia watuhumiwa 36 waliokuwa wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi baada ya kukidhi masharti ya dhamana yaliotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Akizungumza na waandishi wa habari,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi alisema wanamshikilia Mfalme Zumaridi kwa makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Kamanda huyo amesema, Februari 26,2022 majira ya saa 6 na dakika 30 (12:30hrs) huko eneo la mtaa wa Buguku,Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilimkamata Dianna Edward Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi, miaka 39 kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu wapatao 149.

Pia amesema,watu hao wametolewa na kusafirisha toka sehemu mbalimbali kisha kuwafungia nyumbani kwake ambapo alikuwa akiwatumikisha.

Ambapo kati ya watu hao wanaume 57, wanawake 92 na miongoni mwao wapo watoto 24, wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 4-17, ambao wamekatizwa masomo kinyume na sheria.

Kamanda Ng'anzi alidai kuwa, watu hao wamekuwa wakiaminishwa na mtuhumiwa kuwa yeye ni mungu anayeponya,anafufua wafu na ana uwezo wa kutatua matatizo yao.

Amesema, Februari 23,2022 polisi walipokea amri ya Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni iliyotaka kumkamata mzazi wa kike wa mtoto Samir Ally Abbas ayetakiwa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo baada ya kesi ya msingi kusikilizwa.

Katika utekelezaji wa amri hiyo Polisi walifika nyumbani kwa Mtuhumiwa Dianna Edward Bundala ambapo ilidaiwa yupo mzazi wa kike wa mtoto huyo na mtoto aliyetakiwa kufikishwa mahakamani.

Aidha, amesema, baada ya askari kufika eneo la tukio mtuhumiwa akiogoza wafuasi wake waliwashambulia askari na kuwazuia kufanya kazi yao, ndipo askari waliondoka eneo hilo kwa nia ya kuepusha kutumia nguvu ambayo ingeweza kuleta madhara.

"Februari 26, mwaka huu askari polisi walirudi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kufanikisha ukamataji kwa mujibu wa sheria,upelelezi wa kina unaendelea ili kubaini kiini cha watu hao kukusanyika katika nyumba ya mtuhumiwa ambayo sio nyumba ya ibada wala sehemu rasmi ya kongamano.

"Baada ya upelelezi kukamilishwa mtuhumiwa pamoja na washirika wake katika kutenda kosa hilo watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,"amesema.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, jeshi hilo limewaachia watu 36 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi baada ya kukidhi masharti ya dhamana ukiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea kutekeleza maelekezo ya Mwendesha Mashitaka Taifa (DPP) ya kuwaachia jumla ya watuhumiwa 36 wa makosa ya vitendo vya kujihusiha na ugaidi ambao wamekidhi masharti ya dhamana pia tutawaachia watakaokidhi vigezo vya dhamana,"amesema.

Hata hivyo jeshi hilo limetoa wito kwa baadhi ya watu kuacha kutumia mwanvuli wa dini kuwahadaa wananchi wawapo na matatizo ya kijamii hususani magonjwa na hali ngumu ya maisha.

Pia Jeshi la Polisi limewashukuru wananchi ambao waliona viashiria vya kinyonyaji na kutoa taarifa Polisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news