Dubai yaiunganisha Tanzania na fursa kabambe za uwekezaji,biashara

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetia saini Hati za Makubaliano (MoU) 36 wakati wa mkutano wa Biashara na Uwekezaji uliofanyika Dubai.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika leo tarehe 27 Februari, 2022, Dubai, UAE.

Hati 12 kati ya hizo zimetiwa saini baina ya serikali ya Tanzania kupitia wizara na taasisi za umma na wawekezaji mbalimbali wa sekta za umma na binafsi.

Vile vile, hati za makubaliano nyingine 23 zimetiwa saini baina ya makampuni binafsi kutoka Tanzania na makampuni mengine yenye nia ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Hati moja itahusisha Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zanzibar na wawekezaji wanaonuia kushirikiana kwenye sekta ya utalii.
Wafanyabiashara mbalimbali wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wakiwa katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika leo tarehe 27 Februari, 2022, Dubai, UAE.

Idadi ya ajira zinazotarajiwa kupatikana kwa ujumla kutokana na makubaliano hayo ni zaidi ya 200,000 katika kipindi cha miaka minne, huku uwekezaji huo ukigharimu zaidi ya dola bilioni 7.49 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 17.35 za Tanzania.

Sekta zinazotarajiwa kunufaika na hati hizo za makubaliano ni pamoja na nishati, kilimo, utalii, miundombinu, usafiri teknolojia na nyinginezo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na baadhi ya Watanzania Waishio Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) leo tarehe 27 Februari, 2022, Dubai, UAE. (Picha na Ikulu).

Akiongea katika mkutano huo wa Biashara na Uwekezaji, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kushawishi uwekezaji na kutengeneza bidhaa madhubuti na za kisasa, nchi inahitaji elimu bora.

“Leo naisihi hasa Serikali ya UAE na nchi nyingine zinazoshiriki kwenye Expo 2020 Dubai kutoa fursa kwa wanafunzi wa Tanzania kusoma kupitia ufadhili na mpango wa ubadilishanaji wa wanafunzi,"amesema Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news