Rhobi Samwelly atoa ujumbe mzito kuhusu ukatili wa kijinsia mbele ya UWT

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ( HGWT) ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amewaomba wajumbe wa Jumuiya ya UWT katika mikoa mbalimbali wawe mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na ni kunyume cha haki za binadamu. 
Ameyasema hayo leo Februari Mosi, 2022 wakati akitoa mada kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo za kupinga ukatili wa kijinsia katika semina iliyowakutanisha Makatibu na Wenyeviti wa UWT wa Wilaya pamoja Makatibu wa UWT wa Mikoa, Wenyeviti na Wajumbe wa Jumuiya ya UWT Taifa kutoka mikoa mbalimbali katika kikao kilichofanyika makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi Mjini Musoma mkoani Mara. 

Rhobi amesema, viongozi wa jumuiya hiyo katika maeneo yao wanawajibu wa kuendelea kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za serikali za kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu katika maeneo yao kutofumbia macho wahusika wanaofanya vitendo hivyo na kuhimiza usawa miongoni mwa wanajamii. 
Ameongeza kuwa, Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limeendelea kushiriki kikamilifu mkoani Mara kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa njia ya utoaji wa elimu katika shule, mikutano ya hadhara katika vijiji, kuendesha makongamano ya hadhara, kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji, kuwaendeleza kimasomo na kifani mabinti wanaokimbia ukeketaji, kutumia vyombo vya habari kutoa elimu, na kutoa simu janja zenye APP maalumu kwa wanawake ambao hutoa taarifa kupitia simu zao.
"Kina mama wa Jumuiya ya UWT tuna nafasi kubwa sana ya kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ukatili upigwe kwani unarudisha nyuma juhudi za maendeleo, niwaombe katika maeneo yenu ninyi ni viongozi kasimameni kidete kupinga mila zilizopitwa na wakati ambazo hazifai kufanywa kutokana na madhara mfano ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake, na matendo mengine mabaya,"amesema Rhobi.

Pia, Rhobi amewaomba wajumbe hao kuendelea kuwa sehemu ya kufanikisha juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wa kike wanasoma hadi kutimiza malengo yao kwani watatoa mchango mkubwa wa kimaendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla hivyo wasisite kuwaibua watu ambao wanakwamisha malengo ya watoto wa kike. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya UWT Taifa, Gaudencia Kabaka amepongeza kazi zinazofanywa na shirika hilo na pia amesema jumuiya hiyo itaendelea kushiriki vyema kupinga ukatili wa kijinsia. 

Aidha, Kabaka amesema jumuiya hiyo itaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha inazidi kujikwamua kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali na kushirikiana na wadau.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news