TANZANIA YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

NA NTEGHENJWA HOSSEAH,O-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Tanzania inajivunia mafanikio makubwa tangu ichukuwe nafasi ya Uenyekiti kwenye Umoja wa Wizara zinazohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Waziri Bashungwa amesema hayo jijini Arusha wakati akihitimisha Mkutano wa Umoja wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Nchi za Jumiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Februari 7 hadi 9, 2021.

"Katika kipindi hiki tunajivunia umoja huu kwa kuingia hatua ya kusaini makubaliano na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuboresha ushirikiano wa wizara zinazohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndani ya Jumuiya yetu," amesema Mhe. Bashungwa.
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa, katika mkutano huo yamejadiliwa mambo mbalimbali ikiwemo kujitayarisha kwa Serikali za Mitaa kwa ajili ya kufufua uchumi baada ya UVIKO-19 na mitazamo ya jukumu la Serikali za Mitaa, vipaumbele na hatua za kimkakati za EAC.

Waziri Bashungwa amesema kuwa, katika kipindi ambacho Tanzania ni mwenyekiti wa umoja huu itaendelea kukuza mazungumzo kati ya mawaziri na Serikali za mitaa ili kushughulikia changamoto zinazokabili katika ngazi ya mtaa.

Vilevile, amesema Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kurasimisha sekta ya Serikali za Mitaa ndani ya jumuiya hiyo na kuendelea kutoa nafasi ya kubadilishana ujuzi, taarifa, mbinu bora na ubunifu kwa ajili ya utawala wa ndani.
Tanzania ni nchi Mwenyekiti wa Umoja wa Wizara zinazohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) tangu Oktoba 2021 ambapo Umoja huo unaongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa.

Post a Comment

0 Comments