Ubalozi wa Ufaransa: Mambo mazuri yanakuja Tanzania

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

BAADA ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufanya ziara nchini Ufaransa ambayo imekuwa na mafanufaa makubwa,Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajloui amesema ziara hiyo imefungua fursa mbalimbali ambazo zitaendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na kwamba kuna ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara utakuja nchini.
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajloui akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana kupitia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Ufaransa. (Na Mpigapicha Wetu).

Akizungumza leo Februari 18 ,2022 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari Balozi Nabil amesema, katika ziara hiyo Rais Samia na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamepata fursa ya kuzungumza masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo, uchumi na diplomasia.

Amesema, katika mazungumzo yao marais hao pia wamejadiliana kuboresha ulinzi na utunzaji wa bahari ikiwa ni mkakati wa kufikia uchumi wa buluu,miundombinu ya usafirishaji ikiwemo katika majiji makubwa hasa Dar es Salaam na wamezungumzia kuimarisha sekta ya kilimo na uchukuzi.

Pia amesema, marais hao wamejadiliana kuhusu uwekezaji wa biashara kati ya nchi hizo mbili sambamba na kuendelea kukuza diplomasia. ”Tunampongeza Rais Samia kwa kufanya ziara katika nchi yetu ya Ufaransa, kwani imekuwa na mafanikio makubwa, imefungua fursa mbalimbali,"amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu ziara hiyo amesema , anashukuru kuona Tanzania na Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wameingia makubaliano ya kutia saini mikataba mitatu ya miradi ya maendeleo yenye ufadhili wa jumla ya Euro milioni 259.Miradi hiyo itajikita katika sekta ya kilimo, uchukuzi na miundombinu pamoja na vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ya Tanzania.

Balozi Nabil amesema kwamba, nchi ya Ufaransa na Tanzania zitaendelea kushirikiana na hivi karibuni Tanzania inatarajia kupokea jopo kubwa la ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini humo ambapo kwa pamoja watakutana na mamlaka zinazohusika na masuala ya kibiashara kwa lengo la kupanua wigo wa uwekezaji utakaokuza uchumi na maendeleo.

“Wafanyabiashara hao wakiwa hapa nchini pamoja na kukutana na viongozi wa kiserikali watakuwa na ratiba ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu. Wafanyabiara hao kutoka nchini Ufaransa wakiwa hapa Tanzania watakuwa na programu maalumu ya kuwainua wajasiriamali wachanga,”amesema Balozi Nabil.

Rais Samia alikwenda nchini Ufaransa kwa ajili ya kushiriki kilelele cha mkutano wa wakuu wa nchi zilizopo ukanda wa bahari kufuatia mualiko wa Rais wa Ufaransa , Emmanuel Macron.

Pia Rais Samia alipata nafasi ya kuhutubia mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza umuhimu wa yeye kupata elimu inayohusu utawala wa bahari na rasilimali zake.

Rais katika hotuba yake alisema, Tanzania itanufaika kwa kupata teknolojia na miundo bora ya kiuendeshaji wa bahari ili kufikia uchumi wa bluu.

Wakati huo huo Balozi Nabil amekutana na kufanya mzungumza na maofisa na watumishi wa ubalozi huo ambapo amewapongeza kwa kufanikisha na kushughulikia masuala mbalimbali yaliyohusu ujumbe uliombatana na Rais wa Tanzania kufanikisha ziara yake nchini Ufaransa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news