Watakiwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo

NA MWANDISHI MAALUM

WAKATI Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu mbalimbali nchini hasa miundombinu ya kutolea huduma ya afya nchini, wananchi wametakiwa kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miundombinu hiyo ili kupunguza gharama zisizo na lazima lakini pia kuimarisha ulinzi katika miundombinu hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Dionis Myinga alipokuwa akiwasilisha taarifa kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI juu ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ya Afya katika Kituo cha Afya Chekimaji ambacho kinajengwa kwa fedha za tozo za miamala ya simu shilingi milioni 250. 

Amesema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha inaboresha miundombinu hasa ya kutolea huduma ya afya ili kusogeza huduma hizo karibu na jamii hivyo ushiriki wa kila mwananchi utasaidia kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dkt.Irene Haule amesema kuwa fedha hizo zinatumika kumalizia jengo la huduma za nje (OPD) ambalo lipo katika hatua za ukamilishaji , ujenzi wa jengo la mama na mtoto (RCH) pamoja na maabara ambapo majengo hayo yapo katika hatua ya kupaua.

Jengo la OPD lilijengwa kwa nguvu za wananachi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Hai hadi kupaua. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Chekimaji, Selemani Juma ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma ya afya nchini akiamini kwamba jitihada hizo zinalenga kusogeza huduma mbalimbali karibu na jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news