Watendaji wahusishwa na migogoro ndani ya jamii

NA ROTARY HAULE

OFISA oparesheni wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Kibiti katika Mkoa wa Pwani,Grafton Mushi amesema kuwa migogoro mingi inayotokea katika jamii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na watendaji wasio waadilifu na waaminifu.
Mushi alitoa kauli hiyo juzi wilayani humo katika mkutano wa siku moja kuhusu namna ya utatuzi wa migogoro uliowakutanisha wadau wa asasi za kiraia pamoja na waandishi wa habari kupitia mradi wa Jenga Amani Yetu unaoendeshwa na Search for Common Ground kupitia Kituo Sheria na Haki za Binadamu( LHRC) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (European Union).

Amesema, kumekuwa na migogoro mingi katika jamii ikiwemo ya kugombea ardhi,mirathi na hata ya wakulima na wafugaji lakini katika ufuatiliaji imebainika inasababishwa na viongozi wasio waadilifu.

Amesema, ukosefu wa uadilifu huo unapelekea kushindwa kutatua migogoro hiyo na hatimaye kuwanyima haki wananchi jambo ambalo linazua mapigano yanayosababisha watu kuumizana na hata kuuana.
"Rufiji tumekuwa na migogoro ya wafugaji na wakulima lakini migogoro hii ukiifuatilia sana utakuta viongozi na watendaji wa maeneo hayo wasio waadilifu ndio chanzo ndio maana jamii kubwa imekuwa ikipoteza haki,"amesema Mushi.

Mushi amesema, kitendo cha LHRC kupeleka mradi wa Jenga Amani Yetu katika Wilaya ya Rufiji ni wakati muafaka kwa kuwa utasaidia kutatua migogoro inayojitokeza katika jamii na hivyo kulinda haki za wananchi na hata kuleta amani.

"Mradi huu wa Jenga Amani Yetu ulioletwa na LHRC ni mzuri na mimi ningependa uendelezwe katika nyumba zote ili kupunguza migogoro na kuleta amani katika jamii maana bila haki hakuna amani,"amesema Mushi.
Mushi ametoa wito kwa watendaji hao kuhakikisha wanasimamia haki katika utoaji wa maamuzi kwenye migogoro ili kila mwananchi haweze kupata haki yake na kwamba kwakufanya hivyo Wilaya ya Rufiji itakuwa na amani wakati wote.

Kwa upande wake mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambaye ndiye mkufunzi wa mafunzo hayo Ally Seif amesema, mradi huo umelenga kuwaelimisha viongozi wa Serikali,asasi za kiraia na Waandishi wa Habari.

Seif amesema kuwa, lengo kubwa ni kutoa elimu namna ya kupata suluhisho katika migogoro ,kujua mbinu Shirikishi za kutumia katika utatuzi ,kujua madhara ya migogoro na chanzo chake.

Aidha,Seif amesema watu wengi wamejikuta wanaingia katika migogoro hiyo kutokana na kukosa uelewa wa kisheria lakini anaimani kupitia mradi huo wananchi wengi wataelimika.
Hatahivyo,Seif amesema kuwa kila mwanajamii anawajibu wa kulinda amani katika maeneo wanayoishi na kwamba sio kazi pekee ya kuwaachia Polisi, viongozi wa Mtaa na Wanahabari kwakuwa amani ikiharibika haichagui mtu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Dimani iliyopo Wilayani Kibiti Agnes Willa, amesema kuwa mafunzo ya Jenga Amani Yetu yamempa uelewa wa utatuzi wa migogoro katika eneo lake la kazi.

Amesema,katika eneo lake amekuwa akikutana na migogoro mingi hasa ya ndoa hususani kugawana mali ,pamoja na wakulima na wafugaji lakini kupitia mafunzo hayo anaimani yatasaidia kuleta amani na hivyo kupunguza migogoro katika jamii.

Hata hivyo,Agness ameshukuru hatua ya LHRC kupeleka mradi huo katika Wilaya ya Rufiji kwa kuwa mara nyingi wamekuwa na migogoro ambayo wakati mwingine wanakosa mbinu ya utatuzi wake.

Post a Comment

0 Comments