Waziri Bashungwa atoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa kuhusu Mfumo wa Anuani za Makazi

NA ASILA TWAHA,OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewataka viongozi kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia kikamilifu matumizi ya Mfumo wa Anuani za Makazi ili kusaidia upatikanaji wa huduma kirahisi kwa wananchi.
Mhe. Bashungwa amesema hayo Februari 8,2022 jijini Dodoma mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Mfumo wa Anuani za Makazi amesema, Ofisi ya Rais- TAMISEMI imeshirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa maelekezo kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa utekelezaji wa anuani za makazi.

Amesema, kwa majukumu yaliyotekelezwa na Wizara kwa kushirikiana na wadau kuhusu anuani za makazi ni pamoja na kuandaa miongozo ya mfumo wa anuani za makazi, kutunga sheria ndogo, utambuzi wa majina ya mitaa katika Mamlaka za Serikali za mitaa 184 nchi nzima, kuandaa ramani za mipaka ya kiutawala, kujumuisha masuala ya mfumo wa anwani za makazi kwenye mwongozo wa mpango na bajeti katika mfumo wa undaaji wa bajeti.
Mhe. Bashungwa amemuhakikishia Mhe. Rais Samia Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kuratibu na kusimamia anuani za makazi zinatekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau ifikapo Mei,2022 kama ilivyoainishwa katika mpango husika na uandaaaji wa ramani msingi na kuanzia ngazi ya kitongoji, mtaa, kata mpaka Mkoa.

Amezielekeza Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahakikisha zinashirikiana na wadau kuandaa majina ya barabara na mitaa na kuziwasilisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
"Ninazielekeza Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhamasisha wananchi na wadau washiriki katika usimakaji wa nguzo za majina ya barabara na mitaa, kubandika vibao vyenye namba za nyumba na mitaa,” amesema Mhe. Bashungwa.

Aidha, amesema utoaji wa elimu kwa viongozi, watendaji na wananchi kuhusu utekelezaji na matumizi ya mfumo wa anwani za makazi unazingatiwa na amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza maendeleo kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news