WAZIRI DKT.MABULA:TUNAANZA UKAGUZI NA UTAMBUZI WA MAENEO YA UWEKEZAJI NCHINI

MUNIR SHEMWETA NA MAGRETH LYIMO-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula amesema wizara yake itaanza ukaguzi na kuyatambua maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula katika picha ya pamoja na Naibu Waziri, Ridhiwani Kikwete (kushoto) na Katibu Mkuu, Dkt. Allan Kijazi baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza katika wizara yake eneo la Mtumba, kufuatia kuapishwa kushika nafasi hiyo leo Februari 9, 2022. (Picha na Munir Shemweta-WANMM).

Dkt.Mabula ameyasema hayo leo Februari  9,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka kuapishwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘’Maeneo haya lazima tuyafanyie ukaguzi pamoja na kuyatambua hasa yale ya vijijini ambayo ardhi yake inahitaji uhaulishaji ili kupunguza muda wa mwekezaji kusubiri pale anapohitaji ardhi ya kufanya uwekezaji.

‘‘Vipaumbele vya wizara haviwezi kwenda tofauti na vipaumbele vya Rais ambapo Mheshimiwa Rais ameelekeza suala zima la uwekezaji ambapo sisi kama Wizara tutafanya ukaguzi wa maeneo yote yaliyotengwa tuyatambue na tujue wenzetu wa TIC, TAMISEMI, EPZA ardhi walionayo ni kiasi gani na wamepanga kufanya nini,’’ amesema Dkt.Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa wizara na taasisi zake huku akiwa na shada la maua baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza katika wizara yake eneo la Mtumba, kufuatia kuapishwa kushika nafasi hiyo leo Februari 9,2022.
(Picha na Munir Shemweta-WANMM).

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, halmashauri kwa maana ya TAMISEMI kupitia mipango kabambe katika maeneo yao kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na wizara itataka kujua kiasi gani cha maeneo yaliyopo yamepangwa kwa makusudio gani.

Dkt.Mabula ambaye amechukua kijiti cha uwaziri kutoka kwa William Lukuvi alisema, jukumu la Wizara ya Ardhi litakuwa ni kutwaa maeneo hayo ili yawe chini ya Serikali ili mwekezaji atakapofika Serikali itajua sehemu sahihi pa kumpeleka kwa kuwa kutakuwa na kanzidata ya maeneo husika.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiapa mbele ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ikulu ya Chamwino leo Februari 9, 2022.(Picha na Munir Shemweta-WANMM).

‘‘Kwenye maeneo ya vijiji kuna maeneo mengi ambayo yana fursa nzuri za uwekezaji ambapo ardhi ya vijiji inasimamiwa na Sheria Na. 5 ili iweze kumilikiwa inabidi zoezi la uhaulishaji katika maeneo yaliyokusudiwa kuwa ya uwekezaji lifanyike kwa ukamilifu na kuwe na umiliki wa eneo ili mwekezaji atakapokuja tusianze kufanya mikutano ya wananchi ili wakubali,"amesema Dkt.Mabula.

Akigeukia suala la migogoro ya ardhi, Dkt. Mabula alieleza kuwa migogoro ya ardhi inagusa wizara tano za Kisekta na inatokea kwa sababu hapajaweza kuwekewa mpango wa matumizi ya ardhi kwa nchi nzima na kubainisha kuwa, wizara itazungumza na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa maana ya halmashauri zote ili kuweza kuona kwa jinsi gani patakuwa na zoezi la maksudi kabisa la kuhakikisha kwamba walau vijiji na maeneo mengi yanapangiwa matumizi ya ardhi.

‘‘Bila kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi migogoro haiwezi kuisha na tukipanga na kuheshimu makubaliano yaliyowekwa katika maeneo hayo ni wazi migogoro itapungua, ili kufanikisha hili inahitaji ushirikiano wa Wizara Tano za Kisekta,"amesema Dkt.Mabula. 

Kwa upande wa zoezi la anuani za makazi, Waziri wa Ardhi amesema, kipaumbele cha wizara yake itakuwa kwenda kwa kasi kubwa katika suala zima la upimaji maeneo pamoja na kutambua wamiliki wa maeneo hayo.

‘’Kwetu sisi wizara katika zoezi la anuani za makazi limepewa kipaumbele kikubwa kwamba tukizembea tutakuwa tumekwamisha zoezi zima,"amesema Dkt.Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news