TARURA yatoa elimu ya mfumo wa Maegesho Kidigitali kwa viongozi Mkoa wa Morogoro

NA ERICK MWANAKULYA-TARURA

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) leo Februari 9, 2022 umeendesha Semina ya Kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na viongozi wa Mkoa wa Morogoro juu ya matumizi ya mfumo mpya wa ulipaji Ushuru wa Maegesho kwa njia ya Kielektroniki unaotarajiwa kuanza kutumika Machi Mosi, 2022 katika Mkoa wa Morogoro.
Akifungua semina kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja ameipongeza TARURA kwa kuandaa semina hiyo na ameahidi kutoa ushirikiano na kushauri wananchi wapatiwe elimu ya kutosha ili waweze kutumia mfumo huo.
Mfumo wa Maegesho Kidigitali (TeRMIS) ni mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya moto (parking fee), matumizi ya Hifadhi za barabara (Road Reserve User Charges) pamoja na Adhabu kutokana na Ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara.

Mfumo wa Maegesho Kidigitali unadhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali kwani umeunganishwa na mfumo wa GePG ambapo Mtumiaji wa maegesho anapaswa kulipia maegesho baada ya kupatiwa kumbukumbu namba ya malipo (control number) na atatumia Kumbukumbu namba hiyo kulipia maegesho kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala wa Huduma za fedha.
Mfumo huu wa Maegesho Kidigitali umetoa muda muafaka kwa mtumiaji wa maegesho kulipia maegesho ndani ya Siku 14 baada ya kutumia maegesho endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya Shilingi10,000.
Kwa Mkoa wa Morogoro, mtumiaji wa maegesho atatakiwa kulipa Shilingi 300 kwa Saa na Shilingi 1,000 kwa Siku.

Post a Comment

0 Comments