Bidii, maadili, nidhamu ya utumishi wa umma ndiyo nguzo ya mafanikio asema Makamu wa Rais Dkt.Mpango

NA MWANDISHI MAALUM

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo Machi 23, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, mazungumzo yaliofanyika ofisi ya wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais alipokea changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao pamoja mapendekezo na maoni ya watumishi ya namna bora ya kutekeleza majukumu ya wizara hiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala ya Muungano na Mazingira hapa nchini.

Akizungumza na watumishi hao, Makamu wa Rais amewataka kufanya kazi kwa bidii, nidhamu pamoja na kufuata kanuni na maadili ya Utumishi wa umma wakati wote wanapotekeleza majukumu yao. Aidha amewataka kuwa na ushirikiano na Ofisi pamoja na Wizara zingine ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Amesema, wajibu wa wizara hiyo ni kuhakikisha inalinda na kudumisha Muungano hivyo amewataka watumishi hao kuratibu vikao vya kamati ya pamoja vyote kama ilivyopangwa na kutatua changamoto zinazojitokeza pamoja na kuimarisha yale mazuri yote yanayohusu Muungano.

Ameiagiza wizara hiyo kuhakikisha inaongeza kasi ya utoaji elimu ya Muungano kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu, kwa watumishi wa serikali pamoja na jamii kwa ujumla.

Amesema, jamii inapaswa kutambua sifa nzuri za Muungano na kuitaka wizara kutumia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii pamoja na sanaa.

Pia amewataka watumishi wa Idara ya Mazingira kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la mazingira ikiwemo upandaji miti pamoja na usafi wa mazingira. 

Amesema,matatizo kama yaliojitokeza mto Mara hivi karibuni na kusababisha vifo vya viumbe hai katika mto huo yanapswa kutambulika mapema kufuatia ufuatiliaji wa karibu wa mazingira.

Amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa wa mfano katika suala la upandaji miti na kuwataka kuchukua hatua binafsi za utunzaji mazingira katika maeneo wanayoishi.

Pia Makamu wa Rais amewataka kuendelea kufuatilia maazimio ya kimataifa pamoja kuongeza ushirikiano na wadau wa mazingira, sekta binafsi, taasisi za kimataifa , dini pamoja na taasisi za fedha ili kupata teknolojia rahisi pamoja na upatikanaji wa fedha utakaowezesha kutekeleza program mbalimbali za mazingira.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema wizara itaendelea kuwa kioo katika suala la muungano na ajenda ya utunzaji mazingira pamoja na na tayari mafanikio yameanza kuonekana ikiwemo wananchi mbalimbali kuanza uuzaji na upandaji wa miti katika maeneo yao

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news