Jaji Mkuu ahimiza wanasheria kuchangamkia fursa za ajira Afrika Mashariki

*Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa, kuna mwanachama mpya wa jumuiya mwenye watu takribani milioni 90. Je? Wanazuoni wa sheria watatumiaje nafasi hiyo kujenga daraja la kibiashara ili kuendeleza taaluma zao?

NA INNOCENT KANSHA-Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha wanazuoni wa taaluma ya sheria kuchangamkia fursa za tasnia hiyo zinazojitokeza nje ya mipaka ya nchi ili kukuza ushindani na soko la taaluma hiyo hasa kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo na Ujumbe wake (hawapo pichani) mara walipomtemebelea ofisini kwake kwa ajili ya kumsalimu na kujitambulisha jijini Dar es Salaam leo Machi 31, 2022.

Akizungumza na Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, Mhe. Bernard Oundo na Ujumbe wake walipomtemebelea ofisini kwake kwa ajili ya kumsalimu na kujitambulisha jijini Dar es Salaam leo Machi 31, 2022, Prof. Juma amesema Tanzania kama nchi imekuwa mstari wa nyuma kuchangamkia fursa zinazojitokeza nje ya mipaka kwenye tasnia ya sheria.

“Nawasihi wanasheria wa Tanzania kuzitafuta na kuziona hizi fursa za kibiashara zinazoongezeka kila kukicha na kuzitendea haki, nadhani ni wakati muafaka wa kuondokana na uwakili wa karne ya 21 wa kuajiriwa, kuwa na ofisi ya uwakili kukutana na mteja ofisini ili kupata kazi ya kipato,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amesema, taaluma ya sheria inabadilika kulingana na kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo ushindani ni mkubwa na kuna nafasi za kutumia taaluma ya sheria nje ya mipaka kuliko ndani ya mipaka.

“Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa, kuna mwanachama mpya wa Jumuiya mwenye watu takribani milioni 90. Je? Wanazuoni wa sheria watatumiaje nafasi hiyo kujenga daraja la kibiashara ili kuendeleza taaluma zao? Takribani asilimia 80 ya mawakili wanaohitimu kila mwaka nchini hawapati ajira za kudumu,” amesema.
Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kulia) akitia saini kitabu cha wageni Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipowasili kufanya mazungumzo naye, wengine ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea (wa kwanza Kushoto) na Naibu Mhasibu wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Bi. Hafsa Sasya (wa kwanza kulia).

Jaji Mkuu ameueleza Ujumbe huo kuwa yupo tayari kupokea changamoto mpya za kukuza ushindani wa kitaaluma na si kwa Tanzania pekee bali hata nje ya mipaka ili kutengeneza misingi itayoifanya taaluma hiyo kukua na kuchangia kwenye pato la taifa kwa ujumla.

Amebainisha eneo lingine la kuimarishwa kwa tasnia ili kuondoa kikwazo cha kibiashara ni lugha ambayo bado ni kikwazo, hivyo jumuiya inapaswa kuja na agenda ya kutatua changamoto hiyo ya mawasiliano hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 inayotawaliwa na mapinduzi ya nne ya viwanda.

Mhe. Prof. Juma amesema kuwa Kiswahili hakijawezeshwa vya kutosha kiteknolojia ili kiweze kushindana na lugha zingine za kimataifa mfano Kiingereza.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akikabidhiwa zawadi ya kitabu kilichoandikwa na Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki na Rais wa Chama chicho Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kulia).

Kwa upande wake Rais wa chama hicho Mhe. Oundo, alisema madhumuni ya uanzishwaji wa Chama cha wanasheria Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kujenga na kuendeleza taaluma ya sheria, kukuza utawala bora na utawala wa sheria na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanajumuiya.

Pia, Rais huyo alitanabaisha kuwa ujio wake nchini unalenga kuhimiza na kuongeza hamasa kwa wananchama wa Chama hicho Kikanda, kujaribu kuangaza fursa muhimu za kibiashara kwa wanasheria na kuomba ushauri wa namna ya kukuza tasnia ya sheria ndani ya Jumuiya.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akimkabidhi zawadi ya kitabu cha Mpango Mkakati awamu ya pili wa mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 pamoja na machapisho mengine ya Mahakama kwa Rais wa Chama chicho Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kulia).

“Kimsingi tumekubaliana na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Juma kwamba, wanachama wetu waanze sasa kuwa na mtazamo chanya wa kutoa huduma za kibiashara na kuangaza mambo katika wigo mpana wa kuendeleza Jumuiya na sio kutoa huduma kwa kuegemea sera za kitaifa kwa kuangalia fursa za nje ya mipaka”, alisema Rais huyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kushoto) Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea (wa kwanza Kulia) mara walipomtembelea Ofisini kwake.

Aidha, Rais wa Chama hicho akatumia nafasi hiyo kuualika Uongozi wa Mahakama ya Tanzania ili kutoa ushirikiana katika maandalizi ya mkutanao Mkuu wa mwaka wa Chama hicho utakaofanyika mwezi Novemba, 2022 Jijini Arusha na katika mkutano huo kutakuwa na uchaguzi wa kumpata Rais wa Chama hicho ambaye anatarajiwa kutoka nchini Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kushoto) Naibu Mhasibu wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Bi. Hafsa Sasya (wa kwanza kulia) mara walipomtembelea Ofisini kwake.(Picha na Innocent Kansha - Mahakama).

Rais Oundo akamdokeza Jaji Mkuu kuwa Chama chicho kinatarajia tarehe 1 Aprili, 2022 kuendesha mafunzo maalumu ya namna ya kushiriki kikamilifu fursa ya ujenzi wa bomba la Mafuta litakaloanzia Ohima Uganda hadi Tanga Tanzania kwa wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news