Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma yazinduliwa

NA FESTO SANGA-Mahakama Kuu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha amezindua Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma,huku akiwataka wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Uzinduzi huo, ulifanyika katika ofisi za Mahakama hiyo Machi 2, 2022.“Tendeni majukumu yenu kwa mujibu wa sheria na msiende nje ya mipaka yenu,” alisema Jaji Mlacha.

Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha wanabuni njia za kuifanya ijulikane kwa Umma ili wenye malalamiko dhidi ya wakili wajue pa kuyapeleka na kusema kuwa kamati hiyo ijiweke kwenye nafasi ya ulezi wa mawakili.

Baada ya uzinduzi, kamati hiyo ilianza kazi kwa kujengeana uwezo kwa kupitia sheria iliyoianzisha (The written laws (Miscellaneous Amendments) (No.5) Act, 2021 na kujua muundo na majukumu yake.

Akitoa mada katika mafunzo hayo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kuwa sheria iliyoiunda ilianza kutumika rasmi tarehe 11 Oktoba, 2021 tangu ilipotangazwa na Gazeti la Serikali na kuongeza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa kamati hizo za mikoa kulikuwepo na kamati moja tu ya kitaifa ikishughulika na mawakili wote.

Kutokana na idadi ya mawakili kuongezeka kila mwaka, ililazimu kuanzishwa kwa kamati hizo za mikoa ili kuratibu na kusimamia maadili na mienendo ya mawakili katika maeneo husika.

Kwa mujibu wa sheria hiyo wajumbe wanaounda kamati hiyo ni pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ambaye ni Mwenyekiti, Wakili wa Serikali au Mwendesha Mashtaka wa Mkoa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili(Chapter Convener) ambao ni wajumbe. 

Aidha, sheria hiyo inaitaka kamati hiyo kuteua Afisa yeyote mwenye taaluma ya sheria ambaye atakuwa Katibu wa Kamati. Kwa kuzingatia kifungu cha 4 A (2) cha sheria hiyo kamati ilimteua Mhe.Anna Kahungu kwa Katibu wa Kamati.

Aidha, Kamati hizo za Mikoa zinapaswa kutuma taarifa ya utendaji kazi za kila robo mwaka kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news