Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,wadau washirikiana kupanda miti maeneo mbalimbali Karatu

NA SOPHIA FUNDI

KATIKA Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori duniani Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi jana wameadimisha siku hiyo kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali wilayani Karatu mkoani Arusha.
Wadau hao ambao ni Idara ya Utalii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) pamoja na Shirika la Pams Foundation walipanda miti zaidi ya elfu moja katika shule ya Secondari Upper Kitete na katika eneo la korido ya wanyama iliyoko Kata ya Mbulumbulu wilayani Karatu.

Akizungumza na wadau hao mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Wanyamapori na Utafiti kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,Victoria Shayo amesema kuwa lengo la kupanda miti hiyo ni kupunguza mabadiliko ya tabianchi pamoja na mgongano kwa jamii kuingia ndani ya hifadhi kwa kuokota kuni.

Amesema kuwa, kuna wanyama ambao wako hatarini kutoweka kutokana na ujangili pamoja na uharibifu wa misitu unaofanywa na binadamu hivyo kupanda miti hiyo itasaidia wanyamapori kuongezaka kwa kuzaliana, kwani watakuwa mahali salama.
Naye msimamizi wa wanyamapori mwandamizi daraja la pili kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambaye pia ni mtaalam wa miti, Naman N.Naman amesema kuwa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro baada ya kuona kuna mgongano wa jamii kuingia ndani ya ifadhi kwa kutafuta kuni iliamua kuanzisha vitalu vya miti katika Tarafa ya Mbulumbulu na Karatu wilayani Karatu.

Amesema kuwa, mamlaka imekuwa ikisambaza miche bure kwa jamii kwa kuwahamasisha kupanda miti katika maeneo yao ili kupunguza hewa ukaa.
Amesema, kwa sasa tayari wametoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi juu ya umuhimu wa kupanda miti pamoja na kuwasambazia miche ya miti na matunda.

Kwa upande wake Afisa Mhifadhi kutoka TAWA,Audax Mwendabantu alisema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na mti wake shuleni sambamba na kupewa miche mitatu atakayopeleka nyumbani.

Aliwaomba wazazi kupokea miche watakayopelekewa na watoto na kupanda katika maeneo yao lengo likiwa ni kuona Tanzania ya kijani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news