Mara, Maliasili kufanya jambo kumbukizi ya miaka 100 ya Hayati Baba wa Taifa

*Matukio muhimu ya kuenzi tunu, urithi, mawazo na mchango wake thabiti alioutoa kwa taifa kuratibiwa

NA FRESHA KINASA

KATIKA kuadhimisha kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere itakayofanyika Aprili 13, 2022 eneo la Mwitongo Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wamejipanga kufanya matukio mbalimbali muhimu ya kuenzi tunu, urithi, mawazo na mchango wake thabiti alioutoa kwa taifa.
Rais wa Kwanza wa Tanzania, hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. ( Picha na Butiama Gallery/Govt).
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Benjamin Oganga ameyasema hayo leo Machi 26,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutamatika kwa kikao cha Kamati ya Maandalizi ya Mkoa wa Mara kilichohusisha pia watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii huku kikifanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji wa Mkuu wa Mkoa wa Mara uliopo mjini Musoma.

Ambapo wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za umma, binafsi na wananchi kwa pamoja wameaswa kushiriki katika kuenzi mema yote yoliyofanywa na Hayati Mwalimu Nyerere kwa manufaa endelevu ya nchi.

Oganga amebainisha kuwa, Mkoa wa Mara ni mdau namba moja katika kufanikisha jambo hilo, hivyo mkoa umejipanga vyema kwa kushirikiana na wizara hiyo pamoja na wadau wote kufanikisha kwa ufanisi huku akibainisha kuwa, matukio mengi muhimu ya kukumbuka mchango wa Baba wa Taifa yatakuwa yakiendelea kabla ya kufikia Aprili 13, 2022.
Kwa upande wake, Dkt. Christowaja Ntandu ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Kale kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii amesema kuwa, Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengi mazuri na yenye tija kwa taifa ambayo ni vyema kila mmoja akayathamini na kuzidi kuyaishi.

"Tutafanya matukio muhimu kabla ya Aprili 13, siku yenyewe na hata baada ya maadhimisho hayo hii yote ni katika kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere katika masuala mbalimbali kwa nchi yetu, wananchi na taasisi zina nafasi ya kushiriki kikamilifu kuona namna gani Mwalimu aligusa sekta husika,"amesema Dkt.Ntandu.
Naye Afisa Wanyamapori Mkuu, Africo Simon Matogorro amesema kuwa, Wizara ya Maliasili imeendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha Jeshi la Uhifadhi ambalo limekuwa likifanya juhudi kubwa katika kukabiliana na vitendo vya ujangili katika kuhakikisha maliasili na wanyamapori wanalindwa kwa manufaa endelevu ya nchi.

"Mwalimu Nyerere alikuwa mwanzilishi wa uhifadhi, tunatambua vyema tamko alilolitoa mwaka 1961 Mwalimu alitoa tamko la uhifadhi, wizara imeendelea kumuenzi Mwalimu kwa kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii, hifadhi za Wanyamapori zimeongezeka nchini, mapori tengefu, na mengine kupandishwa hadhi kuwa mapori ya akiba.
"Pia kuna mafunzo yanatolewa,kupitia vyuo vya Utalii kikiwemo Pasiansi cha Mwanza, MWECAU na jamii inaendelea kuelimishwa ili maliasi zetu ziendelee kuleta manufaa kwa maendeleo ya taifa," amesema Matogorro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news