Mazungumzo ya Waziri Mkuu Majaliwa, Sheikh Al Thani wa Qatar yaonesha mwelekeo chanya

*Tanzania, Qatar zakubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Khalid bin Khalifa bin Abdulaziz Al Thani ambapo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara ili kukuza uchumi.
“Ninamuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika vikao vyenye lengo la kuimarisha mahusiano kati ya nchi ya Tanzania na Qatar na tumepata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Qatar;

Ameyasema hayo Machi 22, 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Khalid bin Khalifa bin Abdulaziz Al-Thani katika Ofisi ya Waziri Mkuu huyo iliyopo Doha,Qatar.
Amesema, moja kati ya jambo kubwa walilolijadili ni uimarishwaji wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ili kuongeza wigo wa maeneo mengi zaidi ya ushirikiano baina ya mataifa hayo na hivyo, kutumia vema fursa ya kuwa na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia kwa miaka mingi.

Waziri Mkuu amesema kuwa kati ya mambo waliyoyawekea msisitizo ni pamoja na kuimarisha biashara kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Chemba ya Biashara ya Tanzania kupitia ushirikiano na wenzao wa Qatar na kwamba shughuli hizo zitaratibiwa na wizara husika ili kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na kuimarisha mahusiano katika maeneo ya kibiashara na kisiasa pia viongozi hao wamekubaliana kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya elimu ambapo wanafunzi wa Tanzania watapata fursa ya kwenda kusoma Qatar na wa Qatar watakuja kusoma nchini.

Amesema maeneo mengine yaliyowekewa msisitizo katika mazungumzo hayo ni ya sekta za madini na kilimo ili kuhakikisha maeneo hayo ya uzalishaji yanapata wawekezaji wengi. 

“Pia Tanzania ni nchi ya pili yenye mifugo mingi Afrika, hivyo tumewaalika Wa-Qatar waje wawekeze kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ili tupate soko la bidhaa hizo,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news