MHESHIMIWA MARY MASANJA AFUNGA MAFUNZO YA JESHI LA UHIFADHI JIJINI MWANZA

*Ni askari wapya 43 ambao wanajiunga rasmi katika utumishi wa umma

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amefunga mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kwa askari wapya 43 ambao wanajiunga rasmi katika utumishi wa umma, hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Masanja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira kwa vijana hao.

“Kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali vijana na kutoa ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta hii ya misitu ambapo leo vijana 43 wanapewa fursa ya kuitumikia nchi,” amefafanua Mhe. Masanja.
Aidha, amewaasa wahitimu hao kutumia vyema ujuzi na weledi walioupata katika mafunzo hayo ili kulinda na kusimamia vyema rasilimali za misitu.

Pia, amewataka kutunza siri za Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao na kuzingatia viapo vya utii kwa Serikali ili kuendelea kuyalinda maadili na maslahi ya Umma.
Amewakumbusha wahitimu hao kuwa na utu wanapotekeleza majukumu yao kwa kuepuka kutumia nguvu pale isipohitahika hasa wanapokutana na wahalifu katika mazingira yao ya kazi.
Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi yamefanyika kwa watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yaliyolenga kuwanoa maafisa na askari kuingia rasmi katika mfumo wa Jeshi la Uhifadhi ili kusimamia vyema rasilimali za misitu na nyuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news