Mheshimiwa Ndejembi awaachia ujumbe wanakijiji kuhusu barabara inayojengwa na TASAF

*Ni katika Kijiji cha Nange wilayani Misungwi, asisitiza umuhimu wa kuitunza

NA JAMES K.MWANAMYOTO

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wananchi wa Kijiji cha Nange wilayani Misungwi kuhakikisha wanaitunza barabara ya jamii yenye urefu wa kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa, ulioibuliwa na wananchi wa eneo hilo kutokana na uhitaji wa barabara itakayowawezesha kusafiri ili kupata huduma muhimu za kijamii.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi, alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa wilayani humo.
Muonekano wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi, kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa katika wilaya hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasisitiza wananchi wa Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi kuitunza barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF, alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi barabara hiyo wilayani humo.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Nange, mara baada ya kutembelea mradi huo wa ujenzi wa barabara na kubaini uharibifu wa barabara unaosababishwa na wafugaji wa eneo hilo kupitisha ng’ombe kwenye barabara hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema, pamoja na kuwa amefarijika kuwaona walengwa wa TASAF wakifanya kazi ya kujenga barabara hiyo na kupata kipato, lakini wanawajibika kuitunza ili jamii inufaike nayo badala ya kuiacha iendelee kuharibiwa na wafugaji wanaopitisha ng’ombe wao.

“Barabara hii inajengwa kwa fedha za Serikali kupitia TASAF, tukiendelea kuacha ng’ombe wapite na mvua ikinyesha tu itageuka kuwa tope na kuwapa changamoto ya kutokuwa na barabara itakayowawezesha kupata huduma za kijamii kama afya, elimu na usafiri,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Katika kutatua changamoto hiyo ya ng’ombe kupita kwenye barabara hiyo, Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa kijiji kushirikiana na wananchi kutengeneza maeneo ya kupita mifugo pembezoni mwa barabara ikiwa ni pamoja na kuhimiza uzingatiaji wa sheria ya matumizi ya barabara.

Ameongeza kuwa, wananchi wa eneo hilo wanahitaji barabara hiyo isiharibiwe na mifugo ili kuwawezesha akina mama wajawazito kufuata huduma ya afya ya uzazi kwa wakati, wanafunzi wanaotoka umbali mrefu kuwahi darasani na kushiriki masomo kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao baada ya mavuno.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bi. Sarah Mshiu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi, wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji cha Nange kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa katika kijiji hicho.
Mmoja wa walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Nange akishiriki ujenzi wa mradi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa.

Aidha, amewaeleza walengwa wa TASAF wanaonufaika na ujenzi wa mradi huo wa barabara kuwa, ili waweze kuondokana na lindi la umaskini ni lazima miundombinu yao iwe mizuri, hivyo wanapaswa kuhakikisha barabara hiyo inatunzwa na kujengwa kwa viwango bora kulingana na thamani ya fedha.

Kwa upande wake, mlengwa wa TASAF Kijiji cha Nange, Bi. Flora Sospeter amesema, barabara hiyo imekuwa na faida kubwa kwa jamii yao kwani wanapougua inawawezesha kwenda zahanati ya kijiji kwa wakati ili kupata matibabu, tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati barabara ilikuwa mbaya.
Mlengwa wa TASAF Kijiji cha Nange Bi. Flora Sospeter akieleza faida ya barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa.
Mlengwa wa TASAF wa Kijiji cha Nange Bw. Nkiyungu Nkiliga akieleza sababu ya wananchi kuibua mradi wa ujenzi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 unaotekelezwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa.

Naye Mlengwa mwingine wa TASAF wa Kijiji cha Nange, Bw. Nkiyungu Nkiliga amesema kuwa, barabara hiyo ilikuwa ni mbaya sana, hivyo ulivyokuja mradi wa TASAF iliwalazimu kubuni mradi huo wa ujenzi wa barabara ili kusaidia wagonjwa kupata huduma za matibabu na kuweka miundombinu mizuri ya barabara itakayowawezesha kutoa mazao yao shambani.

Barabara hiyo inayogengwa na TASAF katika Kijiji cha Nange kilichopo katika Kata ya Igokelo Wilayani Misungwi inahudumia jumla ya vitongoji 6 vyenye wakazi 3,881, wanaume wakiwa ni 1,746 na wanawake 2,135. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news