Profesa Makubi:Lindeni afya zenu za kinywa

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imewaasa wananchi kulinda afya zao za kinywa na meno kwa kufuata njia sahihi za kujikinga.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Ruvuma.

Prof. Makubi amesema swala la kujikinga na Magonjwa ya Kinywa na Meno ni muhimu zaidi kuliko kusubiri kuingia kwenye hatua ya matibabu.

"Usafishaji wa kinywa kwa usahihi, matumizi ya miswaki yenye sifa stahiki, na udhibiti wa ulaji wa vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kufanya uchunguzi wa Kinywa na Meno walau mara moja kwa mwaka ni miongoni mwa mambo ya msingi na ya lazima ili kuwa na Kinywa chenye Afya njema," amesema Prof Makubi. Aidha, amesema matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku pamoja na unywaji wa pombe uliopitiliza huchangia kupata madhara ya magonjwa ya fizi, saratani kwenye ulimi, mdomoni na koo.

Hata hivyo Prof. Makubi amewahimiza wananchi Kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili kuweza kupata huduma kwa gharama nafuu na haraka.
"Wito wangu kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na taifa nzima tuendelee kujitokeza kwa hiari kujiunga na mfuko wetu wa bima ambao utasaidia kuboresha huduma zetu na kupata huduma bora,"amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha huduma ya Kinywa na Meno zinaimarika, kwa kuendelea kununua vifaa tiba vya kisasa na kuboresha miundombinu ya matibabu hayo katika hospitali na vituo vya afya.
"Takwimu zinaonyesha jumla ya Wagonjwa 685,224 walihudhuria kwa ajili ya matibabu ya Kinywa na Meno katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya kwa mwaka 2021, Wagonjwa 506,950 (74%) walikuwa na tatizo la kutoboka kwa meno ilihali watu 69,318 walikuwa na Magonjwa ya Fizi,"amesema.

Kwa upande mwingine Prof. Makubi amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za afya zina imarika kwa kuendelea kununua vifaa vya kisasa, kujenga miundombinu na kuboresha matibabu kwa ujumla.
"Kwenye fedha za Uviko-19 uwekezaji mkubwa umefanyika katika vituo vyetu vya afya kwa kujenga vyumba vya kutibu wagonjwa mahututi na dharura pamoja na vifaa vya kisasa,"amesema Prof.Makubi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news