Pwani yaja na operesheni MAALUM ya kudhibiti wahamiaji haramu, RC Kunenge atoa onyo kali kwa maafisa Uhamiaji

NA ROTARY HAULE

MKUU wa MKoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amezindua operesheni maalum ya kudhibiti wahamiaji haramu ndani ya mkoa wake huku akiwapiga marufuku maafisa wahamiaji watakaoendesha operesheni hiyo kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Aidha, Kunenge amesema kuwa afisa ambaye atabainika kuchukua rushwa kutoka kwa wahamiaji hao au sehemu yoyote inayohusiana na kuwalinda wahamiaji hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Kunenge ametoa kauli hiyo leo Machi 14,Mjini Kibaha wakati akizindua operesheni hiyo kwa maafisa wa Uhamiaji wa Mkoa wa Pwani huku ikishuhudiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Amesema kuwa,lengo la operesheni hiyo ni kuhakikisha inadhibiti mianya ya wahamiaji wanaoingia katika utaratibu usio rasmi na kwamba zoezi hilo litafanyika katika Wilaya saba na halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani.

Kunenge amesema, wengi wa wahamiaji hao wamekuwa wakijihusisha katika matendo ya uhalifu na hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi wa maeneo husika na kwamba kufanyika kwa operesheni hiyo itasaidia kupunguza vitendo hivyo.
Amesema,kutokana na umuhimu wa zoezi hilo lazima maafisa Uhamiaji wafanye kazi zao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa na kwamba isiwe sehemu ya kuchukua rushwa na kama wanaona wamepewa sehemu ya kuchukua rushwa Serikali haitawaacha salama.

"Natoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt.Anna Makakala kwa kuanzisha operesheni hii, maaana umuhimu wake ni mkubwa hasa katika kuleta usalama wa mipaka yetu na wananchi wetu,"amesema Kunenge.

Kunenge amewaomba wamiliki wa viwanda kutoa ushirikiano kwa maofisa Uhamiaji watakaokuwa wanapita katika maeneo yao ili kusudi waweze kufanya kazi yao vizuri sambamba na kuwasaidia wahamiaji waliopo katika viwanda hivyo kufanya kazi zao vizuri.
"Mimi mwenyewe nitakuwa mstari wa mbele kuongoza operesheni hii siku zote, lakini niwaombe Wakuu wa Mikoa wenzangu watoe ushirikiano wa kubaini Wahamiaji haramu maana haiwezekani wahamiaji wapite mikoa mingine halafu wakamatiwe Pwani,"ameongeza Kunenge.

Kwa upande wake Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Pwani, ACI Omary Hassan amesema kuwa operesheni hiyo ya Siku 10 itaanza leo Machi 14 na kumalizika Machi 23 mwezi huu.

Hassan amesema kuwa, Mkoa wa Pwani kuna wageni wengi ambao wanatoka nchi mbalimbali na kufuatia hali hiyo wapo wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia na hatimaye kufanya vitendo vya uhalifu.
"Kuna athari kubwa za wahamiaji haramu kwa kuwa miongoni mwao hufanya vitendo vya uhalifu na ndio maana Serikali imeona ifanye operesheni hiyo kwa ajili ya kudhibiti wahamiaji haramu, lakini pia kudhibiti vitendo vinavyofanywa na wahamiaji waliopo nchini,"amesema Hassan.

Hassan,amesema kuwa maofisa wa Uhamiaji Mkoa wa Pwani wamejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na anaimani ndani ya muda huo watafikia malengo .

Hata hivyo,Hassan ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanasaidia kuwaibua wahamiaji haramu waliopo katika maeneo yao ili vyombo dola vichukue hatua ya kuwakamata kwa haraka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news