Rais Samia atajwa kupaisha Sekta ya Michezo nchini, wadau wafunguka

>Shule 56 za michezo kujengwa nchini, viwanja vya kisasa

NA GODFREY NNKO 

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa shule 56 za michezo hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea Kombe la Ubingwa wa Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) U23 kutoka kwa Nahodha msaidizi wa Timu ya Taifa ya Vijana U23, Reliant Lusajo tarehe 22 Agosti, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam. (PICHA NA IKULU).

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameyasema hayo Machi 12, 2022 katika mjadala wa Kitaifa ulioangazia Mafanikio katika Sekta ya Michezo Kuelekea Mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.

"Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kujenga shule 56 za michezo, hivyo kwa ushirikiano wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Wizara ya TAMISEMI (Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Wizara ya Elimu (Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia) tayari imeshabainisha shule hizo na Serikali katika bajeti ijayo itatoa shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo,"amesema Mheshimiwa Mchengerwa.

Mjadala huo wa saa mbili na nusu umeratibiwa na Watch Tanzania kupitia mtandao wa Zoom huku ukirushwa mubashara kupitia runinga mtandao mbalimbali kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Mtandao wa Simu wa Airtel Tanzania.

Pia Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amesema kuwa, timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls kushiriki michuano ya kufuzu Kombe la Dunia ni moja wapo ya mafanikio makubwa ya kujivunia kupitia uongozi wa Rais Samia huku akitambua msingi mzuri uliowekwa na Hayati Baba wa Taifa katika kuhamasisha michezo nchini.

"Hatuwezi kutaja mafanikio ya Sekta ya Michezo nchini bila kumtaja Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwani yeye alisisitiza sana katika eneo hili la michezo hasa katika kuibua vipaji na kuongeza ajira kwa Watanzania, eneo hili la Sekta ya Michezo kwa kipindi kirefu sana Watanzania walitamani tupige hatua kama yalivyo mataifa mengine.

"Hivyo, Serikali hii ya Mheshimiwa Rais Samia imejipanga kuhakikisha inaboresha sekta hii ikiwemo ujenzi wa viwanja , vituo vya michezo (academy), kuboresha sera za michezo na ununuzi wa vifaa vya kimichezo na vitu vingine vyote vinavyotakiwa katika kuboresa michezo nchini.

"Katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022 Serikali imejipanga kujenga viwanja vya burudani na michezo katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Geita na takribani shilingi bilioni 10 za Kitanzania na zaidi zitatumika katika ujenzi huo,"amefafanua Mheshimiwa Mchengerwa.

Amesema, kwa upande wa kiwanja cha Dodoma kitajengwa na kitakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji zaidi ya laki moja waliokaa.

"Serikali ya Awamu ya Sita tayari imeshajipanga kufanya ujenzi mpya wa kiwanja cha kisasa kabisa huko makao makuu ya nchi, Dodoma ambapo kiwanja kitabeba watu zaidi ya 105,000,"amesema Mheshimiwa Mchengerwa.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeendelea kutoa nafuu katika ujenzi wa viwanja vya michezo nchini.

Pia amesema kuwa, bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika uagizaji wa nyasi bandia kwa ajili ya viwanja vya michezo nchini.

Dkt.Kigwangalla

Kwa upande wake Mbunge wa Nzega Vijijini, Mheshimiwa Dkt.Hamisi Kigwangalla amesema, mafanikio makubwa yanayoonekana kwa sasa katika Sekta ya Michezo nchini yanatokana na namna ambavyo Mheshimiwa Rais Samia amekuwa mdau mkubwa katika sekta hiyo.

"Rais Samia amepitisha bajeti moja ndani ya Bunge, lakini katika mapendekezo ya Serikali tumeona nia yake ya kuleta mabadiliko na mapinduzi katika Sekta ya Michezo.Na tumemshuhudia mara kadhaa akifanya vikao na kuwatia nguvu vijana wetu wa timu ya wanawake na walemavu. Hii inawapa nguvu kupambana zaidi,"amesema Mheshimiwa Dkt.Kigwangalla.

Kidao Wilfred

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Kidao Wilfred amesema kuwa, kuna neema kubwa ambayo imeanza kuonekana katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yamewekwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

"Ligi yetu (Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara) kwa mara ya kwanza imeanza kuvutia wachezaji wengi wa kigeni. Wachezaji kutoka Zimbabwe, Angola, Uganda, Nigeria, Ghana, Kenya, Rwanda, Burundi wapo katika Ligi yetu ya NBC, huko nyuma wachezaji wetu walikuwa wanatoka kutafuta malisho bora, wao wamegeuza Tanzania kuwa sehemu ya malisho, ni kwa sababu ya uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

"Huko nyuma vijana walikuwa wanacheza mpira kama wa ridhaa, sehemu kubwa ya wachezaji wanawake sasa wanalipwa kama ajira rasmi, jambo ambalo ni kubwa kwa mara ya kwanza watoto wa kike wanaishi kwa kutegemea ajira ya mpira.

"Jambo hili halijawahi kutokea kwa siku za nyuma, kwetu sisi ni mafanikio makubwa mno, pia ndani ya mwaka mmoja ligi kuu hususani ya NBC imekuwa na mafanikio makubwa, kwani wadau wameanza kuwekeza kwenye ligi hiyo,"amesema Bw.Kidao.

Amefafanua kuwa, huko nyuma mapato ya Ligi Kuu kwa wastani yalikuwa shilingi bilioni 7 ndani ya mwaka mmoja, lakini anasema kuwa mapato ya ligi yameongezeka hadi kufikia asilimia 200 ikiwa ni zaidi ya shilingi bilioni 14.

Somoe Ng'itu

Akizungumza katika mjadala huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), Bi.Somoe Ng'itu amesema kuwa, ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani, kumekuwa na ushindani mkubwa katika mpira huo.

"Ushindani umeongezeka sana, mpaka kwa makocha wa kiume kuwania kuomba nafasi ya kuzifundisha hizi timu za wanawake. Hii inamaanisha safari tuliyokuwa nayo kipindi cha nyuma na hii tuliyo nayo kwa sasa ni tofauti.

"Tumefikia kiwango cha juu, kila mmoja anathamini huku kwa sababu kuna jambo, kwa sababu ya hamasa iliyotolewa na Kiongozi Mkuu kwamba mpira huu wa wanawake si tena wa watu wahuni, waliokosa kazi, umekuwa rasmi si tena wa kujitolea kama miaka ya nyuma ambavyo ilikuwa inaonekana,"amesema Bi.Somoe.

Aidha, amesema kuwa, katika kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu ya kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa wamekuwa na ligi mbalimbali.

"Miaka ya nyuma haikuwepo, kwa mara ya kwanza mwaka jana mwezi wa sita tangu Rais aingie madarakani tulipata timu 24 kati ya timu 26 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara ambazo zimeshiriki ligi daraja la kwanza kwetu, ilikuwa ni faraja kubwa sana.Soka letu limekuwa na thamani kubwa kwa sababu tumepewa thamani ile ambayo wanaume walikuwa wanapata,"amesema Somoe. 

KWA WACHANGIAJI ZAIDI TAZAMA HAPA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news