Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania yatoa maelekezo kwa wakulima

NA FARIDA MSENGWA

WAKATI wakulima wakijiandaa kuanza msimu wa kilimo kwa mazao mbalimbali, Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewahimiza wakulima kutumia mbegu zilizothibitishwa ubora.

Sambamba na kukaguliwa na taasisi hiyo ili kupata mazao yenye ubora na kuhakikisha wanapata risiti ili likibainika tatizo iwe rahisi kuwabaini wauzaji feki wa mbegu.
Tayari TOSCI imeshakagua ubora wa mbegu katika kipindi cha mwaka 2020-2021, lengo likiwa ni kupambana na wauzaji wa mbegu zisizo na ubora kabla wakulima hawajazitumia kupanda.

TOSCI imekuwa ikifanya ukaguzi wa mbegu kila mwaka kabla ya misimu ya kilimo, lengo likiwa ni kupambana na wauzaji mbegu feki na wamekuwa wakiufanya ukaguzi huo kwenye maduka,maghala ya kuhifadhia mbegu.

Pia kuangalia wafanyabiashara halali wa mbegu ambao wanatakiwa kuwa na vibali vya kuuzia mbegu na kukagua maghala ya wafanyabiashara wa mbegu ama wazalishaji wa mbegu.

Ukaguzi wa TOSCI ni wa muda wote hata kama ni nje ya misimu ya kilimo huku kaguzi zao zikiwa za kushtukiza.

Vitu muhimu wanavyoviangalia kwenye maghala ni pamoja na kutambua mbegu zilizofanyiwa majaribio ya ubora wa maabara kwa kipindi cha miezi saba.

Kila baada ya miezi saba mbegu inatakiwa kufanyiwa majaribio kutokana na Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

Hivyo mbegu ambazo zimepita muda huo wa miezi saba na hazijafanyiwa majaribio zinafungiwa na zitatakiwa kufanyiwa majaribio na kama zikifanyiwa majaribio na ikabainika hazina ubora zitateketezwa.

Katika uhifadhi mbegu zinatakiwa kuhifadhia katika mazingira yenye ubora, kuwa na uhalali kama amesajiliwa na TOSCI kwa kuwa sheria inataka anayefanya biashara ya mbegu lazima asajiliwe na TOSCI ambapo sheria na taratibu inataka mtu yeyote kabla hajajiingiza kwenye biashara ya mbegu lazima apate mafunzo kutoka TOSCI na kusajiliwa.

Katika majaribio ya uhalisia wa mbegu zilizoko katika uzalishaji katika kipindi cha mwaka 2021, TOSCI iliandaa majaribio ya kutathmini uhalisia wa mbegu zilizoko katika uzalishaji ambapo jaribio Hilo lilihusisha sampuli za mbegu za mazao ya madaraja aina tofauti.

Mazao hayo ni alizeti sampuli 53,ufuta sampuli 13,mtama sampuli 8,mpunga sampuli 11,maharage sampuli 33 na mahindi sampuli 253 kati ya majaribio hayo mbegu za hybrid zikiwa 232 na OPV 21.

Fatuma Nassoro ni mtafiti wa mbegu daraja la 2 wa TOSCI anasema, katika majaribio ya utambuzi wa aina mpya za mbegu katika kipindi cha mwaka 2021 taasisi ilipokea jumla ya maombi 98 kwa ajili ya kufanya majaribio ya utambuzi wa aina mpya za mbegu za mazao mbalimbali ambapo jumla ya majaribio 51 yalifaulu,4 hayakufaulu na 43 yanaendelea kuchukuliwa takwimu.

Aidha, Mtafiti Fatuma alisema katika kipindi cha mwaka 2021 TOSCI imepokea maombi 20 kwa ajili ya kufanya majaribio ya umahiri wa aina mpya za mbegu.

Mazao hayo ni pamoja na mahindi 10,maharage 3,uwele wa malisho1,Mtama wa malisho 3,nyasi za malisho 2,na alizeti 1,huku TOSCI ikiendelea na upandaji wa majaribio hayo katika kanda na maeneo tofauti kama inavyoainishwa katika kanuni ya mbegu.

Fatuma anasema pia katika kipindi hicho hicho cha 2021 taasisi iliendelea kuhudumia,kuchukua takwimu,kuzichakata na kuandaa taarifa za majaribio saba ya NPT ya msimu wa kilimo kwa mwaka 2020/2021 yaliyopandwa katika mikoa ya Njombe, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Songwe, Mbeya, Iringa, Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Lindi.

Mtafiti huyo anasema taarifa za majaribio hayo zinahusisha aina mpya za mazao ambazo ni mahindi 9,ngano 4,ulezi 2, na choroko 2,huku taarifa ya majaribio hayo ikiwasilishwa katika kikao cha 21 cha kamati ya kitaalamu ya majaribio ya umahiri ya kitaifa ya aina mpya za mbegu (NPT-TC).

Katika uchukuaji sampuli za mbegu kwenye maghala mwaka 2021 jumla ya sampuli 2691 kutoka kwenye mafungu ya mbegu (seed lot) yenye uzito wa MT 29,205.2 zilifanyiwa vipimo vya maabara TOSCI Morogoro,Arusha,Njombe na Mwanza.

Kati ya sampuli zilizofanyiwa vipimo hivyo sampuli 2372(88.1%)zilifaulu wakati sampuli 255 sawa na asilimia 9.5 hazikufaulu na sampuli 64 sawa na asilimia 2.4 zilikuwa zikiendelea kufanyiwa vipimo vya maabara.

Katika kipindi cha mwaka 2021 jumla ya sampuli 135 zenye MT 82.7za mbegu (QDS) zilijaribiwa maabara ya TOSCI ambapo kiasi hicho cha mbegu ni sawa na asilimia 5 ya mbegu zote zilizozalishwa nchini kwa mwaka 2021.

Katika mwaka 2021 TOSCI pia ilikagua usajili wa mbegu kwa wafanyabiashara pamoja na makampuni ambapo makampuni ya mbegu yalibainika kusajiliwa,pamoja na wafanyabiashara wa maduka 196.

Katika kipindi hicho hicho pia TOSCI iliendesha zoezi la ukaguzi wa maduka ya mbegu katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe,Tanga na Pwani.

TOSCI iliweza kukagua maduka 367 ambapo kati ya maduka hayo 165 ndiyo yaliyokuwa yamesajiliwa huku 191 hayakusajiliwa na maduka 11 yalifungiwa kwa kosa la kupata mafunzo, lakini hawajaomba kibali cha kuuza mbegu.

Kutokana na hatua hiyo wafanyabiashara wote wametakiwa kufanya biashara ya mbegu kwa kufuata Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2014 pamoja na kanuni zake za mwaka 2017.

Mara baada ya marekebisho ya Sheria ya Mbegu ya mwaka 2014 pamoja na kanuni zake za mwaka 2017, TOSCI ilipewa mamlaka ya kuteketeza mbegu zilizoisha muda wake au zenye viwango duni ama dhaifu vya ubora.

Katika kipindi cha mwaka 2021 TOSCI iliteketeza jumla ya tani za ujazo 279.6 za mbegu,mbegu hizo ziliteketezwa katika Kanda ya Kati na Kaskazini kutokana na mbegu hizo kushuka ubora wake wa uotaji.

UTOAJI WA VIBALI

Katika kipindi cha mwaka 2021 jumla ya vibali 2,333 vya uagizaji mbegu nje ya nchi vilitolewa na TOSCI kwa vituo vya utafiti,makampuni ya uzalishaji mbegu na wauzaji wa mbegu,mbegu hizo zilikuwa kwa ajili ya biashara,majaribio na uzalishaji ambazo kwa pamoja zilikuwa na uzito wa MT 24,246.4 vile vile vibali 12 vya kuuza mbegu nje ya nchi vilitolewa kwa mbegu zenye uzito wa MT 501.8.

TOSCI iliweza kuendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali wa tasnia ya mbegu kuhusu Sheria na kanuni za mbegu pamoja na udhibiti wa ubora wa mbegu jumla ya wafanyabiashara ya mbegu 752 walipewa mafunzo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news