NA FRESHA KINASA
MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema jamii ina wajibu wa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wanaopambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kupigania usawa katika jamii na taifa kwa ujumla.
Rhobi ameyasema hayo leo Machi 6, 2022 wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG kwa njia ya mtandao akiwa nchini Ufaransa.
Amesema kuwa, Serikali imeendelea kufanya vyema katika kuhakikisha vitendo vya ukatili vinamalizika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia hivyo, ametilia mkazo wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa ustawi thabiti wa maendeleo kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi taifa.
"Sote tumeendelea kuona namna ambavyo juhudi za Serikali na mashirika mbalimbali yanavyofanya juhudi kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, nimpongeze Rais Samia kwa kazi nzuri ambazo ameendelea kufanya ikiwemo kuhimiza ushiriki wa wananchi katika kumaliza ukatili, na pia Waziri Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima ameendelea kuwajibika kwa nguvu zote, tumeona ziara mbalimbali akifanya katika vituo vya kulelea watoto yatima, kukutana na wadau, kukemea mila kandamizi na potofu, kuweka mikakati shirikishi ya kumaliza vitendo hivyo juhudi hizo lazima kila mmoja wetu tuziunge mkono,"amesema Rhobi.
"Tanzania tuna neema kubwa kutoka kwa Mungu, Rais wetu amezidi kuliweka taifa letu katika medani nzuri za kutambulika Kimataifa, tumeshuhudia diplomasia ikistawi na ziara zake ambazo amezifanya nje zimeleta matunda kiuchumi na kijamii kwa Watanzania, amewezesha wanawake wengi kuwa viongozi ambao tunawaona wakifanya vizuri sana katika nafasi zao kuongoza kwa weledi mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na maeneo mengine. hii yote ni katika kukuza usawa kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu,"amesema Rhobi.
Rhobi ameongeza kuwa, shirika analoliongoza la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) litaendelea kufanya kazi katika kuhakikisha linachagiza maendeleo ikiwemo kuweka msukumo chanya wa kuwezesha wasichana kusoma ili wafikie ndoto zao, kushirikiana na serikali kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na mila kandamizi ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, na aina nyingine za ukatili ambazo ni kikwazo kwa maendeleo yao.
Machi 8, 2022 ni Siku ya Wanawake Duniani, Rhobi atakabidhiwa tuzo na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kutokana na juhudi zake na kuthaminiwa katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki.