Tanzania, Kenya zakamilisha uwekaji vigingi kutatua mgogoro wa mpaka

>Kamati ya Bunge yapongeza hatua hiyo, yasisitiza utekelezaji huo uendelee maeneo mengine

NA ANTHONY ISHENGOMA

SERIKALI ya Tanzania na Kenya zimekamilisha zoezi la uwekaji vigingi katika mpaka unaoigawa Tanzania na nchi jirani ya Kenya katika Mbuga ya Serengeti na hivyo kufanikiwa kumaliza mgogoro wa mpaka uliokuwepo hususani katika sekta ya utalii kati ya nchi zote mbili.
Miongoni mwa vigingi vya mpaka wa Tanzania na Kenya vilivyowekwa katika Mbuga ya Serengeti mkoani Mara ili kumaliza mgogoro wa mpaka uliokuwepo hususani katika sekta ya utalii kati ya nchi zote mbili.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amesema hayo wakati yeye na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii walipofika katika Mbuga ya Serengeti kujionea utekelezaji huo unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Kikwete amesema, zoezi la uwekaji vigingi katika mpaka huo wenye zaidi ya kilomita 60 utaiwezesha Serikali kupata mapato na sifa ambayo mbuga ya Serengeti iko nayo, akiongeza kuwa vigingi hivyo vimewekwa karibu zaidi tofauti na awali ambapo vingingi hivyo viliwekwa kwa umbali mkubwa na kuwa ngumu zaidi kuvitambua.

‘’Katika kipindi cha mwaka mmoja Serikali ya Rais Samia na ile ya Kenya ziliweza kuingia katika makubaliano ambayo matokeo yake yamewezesha kutatua mgogoro uliokuwepo katika mpaka ndani ya mbuga ya Serengeti na kuleta heshima kubwa kwa nchi zote mbili,"amesema.

Naibu Waziri huyo alitumia fursa hiyo kupongeza mafanikio ya Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja na kubainisha kuwa zoezi kama hilo pia litaendelea kati ya mipaka ya nchi nyingine jirani ikiwemo Uganda, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hasa katika mipaka iliyo ndani ya maji.

Naye Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Ally Makoa amewaagiza watendaji wa wizara kuhakikisha wanatekeleza zoezi hilo na kuharakisha uwekaji vingingi katika mpaka, ili kuondokana na hadha iliyopo katika utambuzi wa mipaka inayoigawa Tanzania na nchi jirani.

“Kazi hii iliyofanyika ni kazi nzuri sana na tunatamani sasa maeneo yetu yote yaliyohifadhiwa yawe na vigingi vya mipaka vinayoonekana kwa malengo yaleyale tuliyoyafanya hapa katika maeneo yote ya nje na ndani ya nchi kuwe na vigingi vivyoonekana ili pasiwe na uvamizi,”Makoa aliongeza.

Wizara ya Ardhi imesema, itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na yale ya kibajeti na kutoa kipaumbele katika utatuzi wa migogoro baina ya nchi jirani kwa kuweka vingingi katika mipaka ambavyo awali viliwekwa na wakoloni katika umbali mrefu na kusababisha sintofahamu katika baadhi ya maeneo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imehitimisha ziara ya kikazi kwa kutembelea programu mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo katika Mkoa wa Singida, Mwanza na Mara.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii katika mpaka wa Tanzania na Kenya ndani ya mbunga ya Serengeti mkoani Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news