Wahasibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi

>Watakiwa kujiongeza kielimu ili kwenda sambamba na wakati uliopo sasa

NA KIJAKAZI ABDALLA-Maelezo

WAHASIBU wa Serikali wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi.
Baadhi ya wahasibu waliyohudhuria semina inayohusu usimamizi na Udhibiti wa Fedha za Umma, huko Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.
(PICHA NA MARYAM KIDIKO/MAELEZO)

Hayo yamesemwa na Mhasibu Mkuu wa serikali, Dkt.Said Seif wakati akifungua semina ya usimamizi na udhibiti wa fedha za umma, hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Kikwajuni.

Alisema, kumekuwa na malalamiko mbalimbali yanayojitokeza katika taasisi zao jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linasababisha kuvuruga mfumo mzima wa utekelezaji wa majukumu yao na kuishushia hadhi tasnia hiyo.

Mhasibu huyo alisema fani ya uhasibu hivi sasa imekuwa na changamoto kubwa ikiwemo kutoaminiwa na badala yake kuonekana watu ambao wanaojali maslahi yao kwanza.

Hata hivyo, alisema kutokana na hali hiyo ipo haja hivi sasa kuwapima watendaji hao kulingana na ripoti ya mkaguzi wa ndani wa hesabu na endapo wakibaini kuna mapungufu ni vyema kujiandaa kuondoka.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, Dkt.Said Seif Mzee akitoa nasaha na maagizo ya usimamizi na udhibiti wa fedha za umma katika semina iliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

"Nimekua nikipokea malalamiko mengine kutoka kwa taasisi na idara tofauti kunitaka kuwaondosha wahasibu katika taasisi zao, hivyo imefika wakati sasa kwa wahasibu kujitambua na kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kujiepusha na hoja zilizokua hazina msingi,"alisema.

Akizungumzia umuhimu wa kutunza siri za ofisi alisema wapo baadhi ya wahasibu wamekuwa wakivujisha siri za taasisi zao jambo ambalo limekuwa likisababisha kukosekana unadhifu na uadilifu.

Mbali na hayo aliwasisitiza watumishi hao kujiongeza kielimu ili kwenda sambamba na wakati uliyopo.

Nae Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ame Burhan aliwataka wahasibu hao kufuata miongozo ya sheria, kanuni na taratibu za kazi zao ili kuondosha changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema zipo sheria na kanuni tayari zimeshapitishwa katika Baraza la Wawakilishi, lakini wapo baadhi ya wahasibu hawazijui hivyo ni vyema kuzifuatilia ili ziwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia taaluma hiyo kwani itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao.

Semina hiyo ya siku moja iliyowashirikisha wahasibu wa serikali na jumla ya mada nne zimewasilishwa ikiwemo udhibiti wa rushwa katika usimamizi wa fedha za umma, maadili na msingi mkuu wa usimamizi wa fedha za umma, majukumu ya kusimamia fedha za umma naudhaifu wa usimamizi fedha katika taasisi za serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news