Waziri Aweso azindua mradi wa uhifadhi, utunzaji maji Karatu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso amezindua mradi wa uhifadhi na utunzaji chanzo cha maji cha chemchem za Qang’dend na mito ya Baray na Mang’ola wilayani Karatu mkoani Arusha.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akikagua birika la kunyweshea mifugo wakati akizindua mradi wa uhifadhi na utunzaji chanzo cha maji cha chemchem za Qang’dend na mito ya Baray na Mang’ola wilayani Karatu mkoani Arusha.

Mheshimiwa Aweso wakati akizindua mradi huo amesema,Serikali kupitia wizara hiyo itatenga kiasi cha shilingi Bilioni nne katika bajeti ijayo inayoanza mwaka huu kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji inayolikabili jimbo la Karatu.

Ayasema hayo wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Kijiji cha Qang’dend kilichopo kata ya Mang’ola Tarafa ya Eyasi wilayani Karatu baada ya kuzindua mradi huo.

Amesema mji wa Karatu ambao ni wa maendeleo, kiuchumi na wa kiutalii unakabiliwa na changamoto ya maji hivyo unahitajika kusaidiwa kupata maji na hasa ukizingatia kuwa hauna umaskini wa vyanzo vya maji kama yalivyo maeneo mengine.
“Nimepata taarifa mahitaji ya maji mji wa Karatu ni lita milioni 5 lakini uzalishaji wa maji kwa sasa ni lita milioni 1.6, Karatu inahitaji kusaidiwa,nataka nikuhakikishie mbunge tunakwenda bungeni katika bunge la bajeti jimbo la kwanza kuliangalia itakuwa ni Karatu na katika bajeti tutatenga Sh.4 Bilioni kutatua tatizo la maji,”amesema.

Amesema, kumekuwa na changamoto katika suala la fedha zinazotolewa na serikali hivyo wataalamu wa Karatu wafahamu kuwa serikali haileti fedha hizo kwa ajili ya kuziweka mfukoni halafu matokeo hayaonekani,hapana.

“Tumewahi kusema na tunaendelea kusema vipo vya kuchezea ukishiba chezea kidevu au kitambi chako si fedha za miradi ya maji, tutakushughulikia na mimi bwana ni kijana ukinizingua tunazinguana, ..wabunge hizi ni fedha na wala hazina mjadala twendeni tukazisimamie ili wananchi wanufaike na upatikanaji wa maji,”amesema Mheshimiwa Aweso.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akipanda kwenye tenki la maji kwa ajili ya kulikagua baada ya kuzindua mradi wa uhifadhi na utunzaji chanzo cha maji cha chemchem za Qang’dend na mito ya Baray na Mang’ola wilayani Karatu mkoani Arusha.

Waziri Aweso amewagiza viongozi wa mabonde yote ya maji nchini kuhashirikisha wanawashirikisha wananchi katika suala la kulinda na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo.

“Jamii ukiishirikisha utafanikiwa, jamii usipoishirikisha utakwama,kwa hiyo watu wetu wa raslimali za maji niwaombe suala la kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na bonde wananchi wanahitaji kushirikishwa,”amesema.

Ameongeza kuwa, asilimia kubwa ya viongozi na hata wananchi wanajua umuhimu wa kujengewa mradi tu, lakini wanasahau suala la kulinda na kutunza vyanzo vya maji.

“Hatuwezi kuona leo shughuli za binadamu zinafanyika katika vyanzo vya maji, hatuwezi kuona uchimbaji madini unafanyika katika vyanzo vya maji mtu wa bonde leo upo tu ofisini umekaa huwezi kuona,lazima ushirikishe jamii na viongozi wa eneo husika,”amesema.

Mheshimiwa Aweso amesema haipendezi na wala haifurahishi kuangalia katika runinga mwananchi ameshalima mazao yake kwenye chanzo cha maji halafu afisa wa bonde anakwenda na panga kuyakata kwani wakati mwananchi analima huyo afisa alikuwa wapi.

“Hivi karibuni na ninyi ni mashahidi hali iliyoikumba jiji la Dar es Salaam kwenye vyanzo vya maji vya Ruvu chini na juu vilikauka kabisa jiji la Dar es Salaam likawa halina maji kabisa mimi Waziri wa Maji nikaona kwa hapa ilipofikia natakiwa niitwe waziri wa ukame,”amesema.

Aweso amesema, wananchi lazima watambue kuwa suala la mazingira lina kisasi ambapo ukiyaharibu mazingira na wewe yatakuharibu na ukiyatunza na wewe yatakutunza hivyo hakuna asiyejua maji chanzo kikibaribika kitapotea na mateso yake ni makubwa.

Amesema miaka ya nyuma maeneo mengi yalikuwa na chemchem za maji lakini leo hii hazipo zimekauka kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi kwa kulima katika vyanzo vya maji na kuendesha shughuli za ufugaji.

“Niwaombe sana ndugu zangu maji ni uhai, maji hayana mdabala, maji si kama wali ambao ukikosa wali unaweza ukala ugali,ukikosa ugali unaweza ukala ndizi, mtu anauyekosa maji maana yake anakaribisha maradhi,”amesema.

Hata hivyo, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Bodi ya Maji Bonde la Kati ya kutekeleza mradi huo, Waziri wa Maji, Aweso alitangaza kumpandisha cheo aliyekuwa akikaimu nafasi ya Afisa Maji Bonde la Kati, Danford Samson kuwa Afisa Maji Bonde la Kati.

“Huyu Kaimu Afisa Bonde ya Maji Bonde la Kati ‘Danford Samson’ ukimwangalia mpole unaweza ukawa na mashaka juu ya utendaji wake wa kazi, kwa heshima na taadhima naomba leo nimteue awe Afisa Maji Bonde la Kati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya akishirikiana na wafanyakazi wenzake,” amesema.
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Dkt.George Lugomela amesema, hapa nchini kuna jumla ya vyanzo vya maji 1,867ambavyo vinatoa huduma, lakini vipo katika hatari ya kuharibiwa.

Dkt.Lugomela amesema, vyanzo vya maji ambavyo vimewekewa mipaka ni 180,vilivyotangazwa katika Gazeti la Serikali na kupata GN ni 18 na vyanzo 45 vipo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali vinasubiri kwa ajili ya kutangazwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news