Waziri Dkt.Nchemba: Mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, tumepiga hatua kubwa kiuchumi

*Asema ukuaji wa uchumi umeanza kuimarika na kufikia asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 mwaka 2021

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema katika siku 365 za Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania madarakani kumekuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi hapa nchini.
Mhe. Nchemba ameyasema hayo leo Machi 15, 2022 jijini Arusha wakati akitoa taarifa ya ya siku 365 za Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania kwa wahariri na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Hazina ndogo jijini Arusha.

Amesema, kutokana na sera bora za Mhe. Rais Samia tangu aingie madarakani Machi 2021 Ukuaji wa Uchumi umeanza kuimarika na kufikia asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 mwaka 2021.

“Kama mtakumbuka ukuaji wa uchumi ulishuka baada ya UVIKO-19 kutoka asilimia 7.0 hadi 4 na baadaye 4.8 mwaka 2020 na sasa ukuaji umepanda tena kutoka asilimia 4.8 hadi 4.9 na matarajio katika kipindi kijacho ukuaji huo utapanda hadi asilimia 5 na wenzetu wa Benki ya Dunia wanatabiri uchumi wetu utakuwa kwa zaidi ya asilimia 5.5,”amefafanua Dkt. Nchemba.

Amesema, kimsingi mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati katika sekta za Nishati, Maji, Afya Elimu, Ujenzi wa Barabara, Reli, Viwanja vya Ndege pamoja na maeneo mengine yaliyochochea ukuaji wa uchumi, mfano Madini, Makaa ya Mawe na uzalishaji wa shughuli za kilimo.

Pamoja na mwenendo huo kukua kwa pato la taifa, lakiini kuna maeneo mahsusi ambayo yameonyesha tofauti tangu Mhe. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ni pamoja na ongezeko la mikopo kwa sekta binfasi na kufikia asilimia 10 Desemba 2021 kutoka asilimia 3.3 Desemba 2020.

“Ongezeko hili ni kubwa sana, maana yake kuna shughuli zimefanyika kwenye sekta binfasi na kama kuna shughuli zimefanyika kwenye sekta binafsi maana yake ajira zimeongezeka kwenye sekta binfasi na kama ajira zimeongezeka kwenye sekta binfasi binafsi maana yake ongezeko hilo linagusa mpaka familia ya mtu mmoja mmoja,”amefafanua Mhe. Dkt. Nchemba.

Nyingine ni Serikali ya Awamu ya Sita kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, hususan utashi wa kisiasa wa kufanya majadiliano na wawekezaji wa ndani na nje; kasi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo; kuendelea kuishirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi; na utekelezaji wa mpango wa kukabiliana na athari hasi za UVIKO-19 (Tanzania COVID-19 Socio-economic Response and Recovery Plan – TCRP).

Kisekta Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, Rais Samia ameweka kipaumbele katika kuhakikisha huduma za jamii zinaimarika na kuwa bora zaidi.

Katika sekta ya Afya amesema, Serikali imeendelea na ukamilishaji wa ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa 19; kuendelea na ujenzi wa Hospitali 127 za Halmashauri ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji; kuendelea na ukamilishaji wa zahanati 564, ikiwa ni wastani wa maboma matatu (3) kwa kila Halmashauri; Kuendelea na ujenzi wa vituo vya afya 233 katika Tarafa 207 zikiwemo Kata za Kimkakati vyenye uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji ambapo majengo yanayojengwa ni Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), Jengo la Maabara na kichomea taka.

Aidha katika sekta ya Maji, Rais Samia pia aliweka mkazo Upatikanaji wa huduma ya maji hadi Desemba 2021 umefikia wastani wa asilimia 72.3 vijijini kutoka asilimia 70.1 Desemba 2020 na mijini asilimia 86 kutoka asilimia 84 mtawalia.

“Katika hili Kazi zilizofanyika ni pamoja na: ukarabati wa vituo 101 vya kufuatilia mwenendo wa maji; kukamilika kwa utekelezaji wa miradi 249 ambayo imeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 1,115,056 waishio vijijini,”amefafanua na kuongeza

"Kuendelea na utekelezaji wa mradi wa maji na usafi wa mazingira Arusha ambapo utekelezaji umefikia asilimia 73; kuendelea na utekelezaji wa mradi wa maji na usafi wa mazingira mji wa Kigoma ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95; kukamilika kwa utekelezaji wa Mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Longido; kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Maji Orkesumet ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 98.5; na kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 31. Jumla ya shilingi bilioni 292.51 zimetumika,"amesema.

Kwa upande wa Elimu nako Rais amefanya makubwa ikiwa ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Chuo kikubwa cha Ufundi Dodoma ambapo shilingi bilioni 3.44 zimetumika. Kadhalika shilingi bilioni 304.0 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 3,000 katika shule shikizi za msingi, madarasa 12,000 katika shule za sekondari na mabweni 50 ya shule za wasichana na shilingi bilioni 47.8 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 25; Ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika Mkoa 4 vya VETA ambayo haikuwahi kuwa na vyuo vya VETA ambayo ni Geita, Njombe, Rukwa na Simiyu.

“Bila kusahau Serikali inaendelea na utekelezaji wa programu ya Elimumsingi Bila Ada ambapo jumla ya shilingi bilioni 137.3 zimetolewa kati ya Julai hadi Desemba 2021; na kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 326.56 kwa wanafunzi 149,472 wa Elimu ya Juu na kuwarudisha shuleni wanafunzi wa kike walioachishwa masomo kwa changamoto mbalimbali,”amesema.

Kuhusu Miradi ya Kimkakati Waziri alisema, Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR) ambapo kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 95.3, Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 81.1; Mwanza – Isaka (km 341) asilimia 4.02 lakini pia kumesainiwa mkataba wa ujenzi wa njia ya reli kwa kipande cha Makutupora – Tabora (km 368).

Aidha, Serikali imekamilisha mchakato wa kumpata Mkandarasi wa kipande cha Tabora -Isaka (km 163) pamoja na kukamilisha taratibu za kuanza mchakato wa kumpata mkandarasi wa kipande cha Tabora – Kigoma (km 514).

Halikadhalika alisema Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115: Kwa ujumla utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 55.3.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news