Agizo la Rais kuhusu kupima watumishi kupitia TEHAMA latekelezwa

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama wamebainisha utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuitumia mifumo ya TEHAMA katika kupima utendaji serikalini ili kuimarisha uwajibikaji na utoaji Huduma bora.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Joyce Ndalichako (Kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Kushoto) wakiwa katika Mkutano na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuhusu mtazamo wa serikali ya Awamu ya sita katika Uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na Matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji na utoaji Huduma bora katika Utumishi wa Umma,tarehe 9 Aprili, 2022 Jijini Dodoma.

Wakiongea tarehe 9 Aprili, 2022 Jijini Dodoma, wakati wa mkutano na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuhusu mtazamo wa serikali ya Awamu ya sita katika Uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na Matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji na utoaji Huduma bora katika Utumishi wa Umma, wamefafanua kuwa serikali inaendelea kufanya maboresho ya kisekta na mtambuka ya kujenga mifumo ya TEHAMA.

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa pamoja na juhudi za serikali za kupima utendaji kazi serikalini Mhe. Rais amelekeza ushirikishwaji wa Vyama vya Wafanyakazi amewataka Vioongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuendelea kuwa daraja kati ya waajiri na Wafanyakazi kwa kuchochea na kuhimiza utamaduni kwa Wafanyakazi kudai haki na kutimiza wajibu wao.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu imeendelea kutekeleza maagizo ya Mhe, Rais kwa kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji wa Vibali vya Kazi kwa raia wa kigeni. Mfumo huo umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku za kazi 14 hadi siku 7. Aidha, Mfumo huo umeimarisha uwazi na uwajibikaji.

Kwa upande wake Mhe. Mhagama amebainisha kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora amefafanua kuwa Ofisi hiyo imetekeleza maagizo ya Mhe. Rais kwa kujenga na kufanya maboresho katika mifumo ya Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS), Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi (PIPMIS).
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya (wa kwanza kulia ) akifuatilia Mkutano na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuhusu mtazamo wa serikali ya Awamu ya sita katika Uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na Matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji na utoaji Huduma bora katika Utumishi wa Umma,tarehe 9 Aprili, 2022 Jijini Dodoma.

Mhe. Mhagama amebainisha kuwa mifumo mingine ambayo imetekelezwa na Ofisi hiyo kuwa ni; Mfumo wa e-mrejesho, Mfumo maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu, Mfumo wa Huduma Mtandao kwa Watumishi (Watumishi Portal) pamoja na mfumo wa SEMA NA WAZIRI.

Ameongeza, Mhe. Mhagama amesisitiza kuwa utekelezaji wa maagizo hayo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Dira na maono yake yanakamilika ambapo anapenda kuwa na Utumishi wa Umma unaofanya kazi kwa: Uadilifu; Uwajibikaji; Bidii na Weledi; Haki na Uzalendo wa Kitaifa.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), Rashid Mtima (Kushoto) akifuatilia Mkutano na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuhusu mtazamo wa serikali ya Awamu ya sita katika Uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na Matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji na utoaji Huduma bora katika Utumishi wa Umma,tarehe 9 Aprili, 2022 Jijini Dodoma. (Picha na OWM-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu).

Amewataka Viongozi wa Wafanyakazi pamoja na kusimamia haki na maslahi ya Watumishi wa Umma kuhakikisha wanawasimamia Watumishi wa Umma ili kuhakikisha wanachapa kazi kwa utalaam, ubunifu, weledi wa hali ya juu na kwa kuzingatia maadili ya utendaji katika Utumishi wa Umma ili kufikia Dira, Maono na Azma ya Kiongozi Mkuu wa Nchi yetu.

Katika hatua nyingine, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wamewapongeza Mawaziri hao na kuipongeza serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kujenga mifumo mipya ya TEHAMA inayoimarisha Utumishi wa Umma wa uwajibikaji wa hiari, hali hiyo imeonesha dhamira ya dhati ya serikali ya kuwajali wafanyakazi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news