Balozi Mbega akaribisha wawekezaji kutoka India

NA DIRAMAKINI

BALOZI wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali za uwekezaji.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa kongamano hilo.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akiongoza kikao baada ya uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wa biashara na uwekezaji ITTC.

Alitoa wito huo katika kongamano kubwa la biashara na uwekezaji (Tanzania India Trade Conference) lililofanyika katika jiji la Chennai, India tarehe 11 na 12 Aprili 2022.

Kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini India na Taasisi ya Uchumi na Biashara ya India (Indian Economic Trade Organization) lilitoa fursa kwa taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara ikiwepo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega akikata utepe na kuwasha mshumaa kuashiria uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wabiashara na uwekezaji ITTC.

Balozi Mbega alisema licha ya India kuwekeza nchini mtaji wa kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 3.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa ya tano kwa uwekezaji, lakini bado nchi hiyo ina fursa kubwa ya kuongeza uwekezaji wake nchini.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wafanyabiashara na wawekezaji takribani 110 ambapo waliweza kufahamishwa fursa za biashara kwa bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na fursa za uwekezaji katika sekta za Miundombinu, Madini, Ujenzi wa majumba, viwanda vya madawa, mitambo ya viwandani, nguo, Elimu na Afya.

Kutokana na kongamano hilo, tayari wawekezaji mbalimbali wa India wameonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania ambapo kundi la kwanza la wawekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa viwanda vya madawa ya binadamu na vifaa tiba kutoka India, linatarajiwa kutembelea Tanzania kuanzia tarehe 19 Aprili 2022 ili kukutana na wadau na kuanza taratibu za kuwekeza Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akifungua Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India Jijini Chennai, India.

Wafanyabiashara wengine walioshiriki Kongamano hilo wameonesha nia ya kushiriki maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam ambayo yataanza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2022. Ushiriki huo utawawezesha kukutana na wafanyabiashara na kuona bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania.
Mada kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania.

Kupitia kongamano hilo, wazalishaji wa bidhaa za Ngozi na korosho wa Tanzania wameunganishwa na wafanyabiashara wa India ambapo watapata fursa ya kuuza bidhaa hizo katika soko la India.

Sambamba na kongamano hilo, Ubalozi pia ulishiriki katika hafla ya uzinduzi wa ofisi ya uhamasishaji na uratibu wa biashara na uwekezaji inayojulikana kwa jina la INDIA TANZANIA TRADE COMMISSION (ITTC) iliyopo katika jengo laJJ Diamonds Mart No. 85, Barabara ya Gopathi Narayanas wani Chetty Chennai katika eneo la Thyagaraya Nagar ambalo ni kitovu cha biashara jijini Chennai. Ofisi hiyo itaongozwa na kusimamiwa na Dkt. J. Shrenik Naharkama Kamishna wabiashara wa ITTC.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na India katika hafla ya uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wabiashara na uwekezaji ITTC.

Uwepo wa ITTC utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haraka wa taarifa sahihi za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kwa kuwa ITTC itakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na taasisi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji za nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news