BARRICK yapigwa faini Bilioni 1/- uchafuzi wa mazingira Mara,Afisa Migodi Mkazi aondolewa

NA TITO MSELLEM-WM

KAMPUNI ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Dhahabu wa Barrick kupitia mgodi wake wa Barrick North Mara umepigwa faini ya shilingi bilioni moja baada ya kutokea uzembe uliopelekea bomba la maji taka kupasuka na kutiririkia kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick kwa asilimia 84 na Serikali kwa asilimia 16 unapaswa kuwa mfano bora kwa kufuata na kusimamia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa na serikali.
"Haiwezekani bomba la maji taka lipasuke saa tatu asubuhi halafu uongozi upate taarifa saa sita mchana na isitoshe kuna walinzi wanaozunguka maeneo hayo, huu ni uzembe wa hali ya juu, sisi tunataka usalama wa watu wetu,"amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amembadilishia majukumu Afisa Migodi Mkazi wa Mgodi wa North Mara baada ya kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo katika eneo alilopangiwa.
"Kutokana na uzembe huu uliofanyika hapa mgodini naanza na Afisa wangu namuondoa hapa ataenda kupewa majukumu mengine, siwezi kukubali uzembe huu uendelee," amesema Dkt. Biteko.

Sambamba na hayo, Waziri Biteko ameitaka Kampuni ya Barrick kuhakikisha inachangia katika kuleta maendeleo kwa jamii (CSR) ili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka Migodi yaweze kunufaika na uwepo wa mgodi huo katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka amesema, Kifungu cha 187 cha Sheria ya Mazingira kinampa mamlaka ya kuipiga faini yenye makosa ya kuvujisha maji taka kuanzia milioni 50 mpaka bilioni 10.
"Kampuni hii ya Barrick tumeipiga faini ya bilioni moja ili iwe mfano kwa wengine, hivyo itambuliwe hilo ni kosa na sisi kama NEMC tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha makosa kama haya hayajitokezi," amesema Dkt. Gwamaka.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Happy amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anataka kuona fedha zinatolewa kwa ajili ya miradi inawanufaisha wananchi ambapo ameitaka kampuni ya Barrick kutoa michango yake kwa jamii (CSR) ili kusogeza maendeleo kwa jamii.
Pia, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mwita Waitara amempongeza, Dkt. Biteko na kusema tatizo la kupasuka kwa bomba la maji taka limetokea jana lakini leo Waziri mwenye dhamana amefika eneo la tukio, hiyo inaonyesha ni kiasi gani anajali na anathamini utu wa watu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news