Dawa za kulevya zilivyoacha kilio kwa Mtumishi wa Umma Shirika la Posta

NA GODFREY NNKO

"Basi pale kazini kulikuwa na mfanyakazi mwenzagu, yeye alikuwa kwenye 'Strong Room', nikawa ninafanya ujanja ujanja, nina-edit (kuhariri), ninafuta, halafu ninatuma, anafanya mahesabu ya mwisho, yeye ana-balance, tunagawana fedha, ninakwenda kununua unga (heroine), nilifanikisha hilo kwa sababu mimi ndio nilikuwa na password ya system (neno siri la mfumo wote) yote;

Yohana Komba ambaye alihudumu nafasi ya utumishi wa umma katika Shirika la Posta Mkoa wa Tabora kwa miaka karibu sita kati ya mwaka 2007 hadi 2012, akiwa amebobea zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari (IT) na kuachishwa kazi kutokana na matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kulevya ameyasema hayo katika mahojiano maalum na DIRAMAKINI BLOG.

Akiwa ni mtu ambaye anaonekana kujutia katika maisha yake, Bw.Komba anasema utumiaji wa dawa za kulevya umemuathiri kiuchumi, kisaikolojia, kiafya, kifamilia na kijamii ikiwemo kumjengea taswira mbaya katika utumishi wa umma.

Yohana Komba ni nani?

Huyu ni Mtanzania aliyezaliwa Julai 11, 1980 katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru miaka hiyo, wakati baba yake akifanya kazi katika Kiwanda cha General Tyres.

Kuhusu General Tyres

Mwanzoni mwa mwaka 2015, mwandishi wa makala haya akiwa katika moja ya ziara iliyoongozwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi.Janeth Mbene jijini Arusha tulielezwa kuwa, General Tyres East African Limited (GTEA) kilikuwa moja wapo ya viwanda vikubwa zaidi nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki.

Na kiliwahi kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha kutengeneza magurudumu katika ukanda wa Afrika Mashariki kikiwa na uwezo wa kuzalishaji magurudumu 1,200 kwa siku na kiliajiri wafanyakazi 4,000.

GTEA kilianza uzalishaji mwaka 1971 na kilibadilisha umiliki mara kadhaa mwishoni mwa miaka ya 1990 na katikati ya miaka ya 2000 wakati General Tyres Amerika Kaskazini ilipouza hisa kwa kampuni ya Continental AG ya Ujerumani na kiwanda hicho nchini Tanzania kufungwa kutokana na kuongezeka kwa uagizaji wa magurudumu kutoka nje ya nchi kutoka kwa wasambazaji wengine wa Kimataifa.

Pia Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lilikuwa limeanza kazi ya kukarabati majengo ya kiwanda hicho na maeneo ya jirani ikiwemo kufanya uhakiki wa kiwanda hicho, kwani mashine zilikuwa katika hali ya kufanya kazi. Hapo ndipo, baba yake, Yohana Komba alipokuwa anafanya kazi, nini kilijiri, kwa kuwa kusudi letu si kufahamishana kuhusu kiwanda, tuendelee na yanayomuhusu Yohana;

"...mzee wangu alikuwa anafanya kazi General Tyres Arusha nilipofika darasa la tatu kwenye miaka ya tisini hivi,sikumbuki vizuri maana haya madawa yaliniathiri sana kimwili, kiakili na kijamii ila ninamshukuru Mungu fahamu zimerudi, maana kurudi kwenye utimamu ni mchakato mrefu, maana sijavuta jana wala leo, nilivuta sana.

"Mara nyingi ukiwa kwenye mchakato wa kuvuta unakuwa na vijitabia vibaya, hata darasani kukaa back bencher, wizi, kuchelewa nyumbani nilijichanganya na makundi mabaya siambiliki"

Wahamia Dar

Anasema, kuanzia mwaka 1990 walihama jijini Arusha kwenda Dar es Salaam, "Basi kipindi hicho tulihamia Dar es Salaam, tumekaa pale Kinondoni, makuzi yangu ni Dar es Salaam ambapo kuanzia darasa la tatu mpaka darasa la saba nilimalizia Dar es Salaam, ndipo nilipoanza matumizi ya bangi nikaenda nayo Shighatini Secondary School iliyopo Ugweno katika Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro huko ndani ndani kidato cha kwanza, basi nikiwa huko kijijini nilijiona mjanja.

"Nilijisikia fahari kujiona nimetoka mjini, ilikuwa mwaka 2000 mwanzoni, nikiwa hapo shuleni nikajihusisha na makundi mabaya huku tukivuta bangi, hatimaye wakanikamata, nikafukuzwa mwaka wa kwanza kabisa.

"Baada ya kufukuzwa nikaenda Shule ya Kiriki haipo mbali sana ni jirani, na tabia zangu zikaendelea vile vile nikaingia fomu two, sikukaa hata mwaka wakanifukuza tena nikaenda Dar es Salaam nyumbani,basi mzazi wangu kwa maana ya mama akanitafutia shule nyingine Mbeya ya Lutengano Sekondari, nikaanza fomu three hadi form four.

Makundi mabaya

"Lakini tabia zangu zilikuwa vile vile, nikajiingiza kwenye makundi na kuvuta bangi, hatimaye walinikamata na bangi nikafukuzwa shule ilikuwa nimebakiza kama mwezi mmoja kufanya mtihani, wakamuita mama yangu nikatangazwa mstarini, nikawa nimefukuzwa shule, nikarudi nyumbani ilikuwa mwaka 2003.

"Tukarudi Dar es Salaam, kwa hiyo mwaka huo sikufanya mtihani, basi mama yangu akawa amenitafutia shule nyingine Dar es Salaam pale Kinondoni, nikafanya mtihani mwaka uliofuata, lakini tabia ni zile zile nikawa na marafiki na ukizingatia ni mjini kuna marafiki tofauti.

Utumiaji Heroine

"Nilipata rafiki mmoja ambaye anatumia unga (Kinondoni Dar es Salaam) akawa anavuta na mimi kidogo kidogo nikaanza kuwaza kuacha bangi nikavuta unga ili nisionekane mshamba, safari ya kuvuta unga (heroine) ikaendelea na ilikuwa mwaka 2005 hivi,basi nikafanya mtihani matokeo yakatoka hayakuwa mazuri nikapelekwa Chuo cha VETA nikasoma mambo ya Information Technology (IT).

"Baadae nikaenda The University of Dar es Salaam Computing Centre (UCC) pale Mlimani City, nikasoma Information Technology upande wa Networking, nikajikita zaidi kwenye upande wa kushoot (troubleshooting) nikamaliza, nikasoma programu nyingine muhimu sana, huwa inapaswa usome online na ufanye mtihani kwenye online World wide. Unapaswa upewe beji unapofaulu na inatambulika ila unalipia dola mia kufanya mtihani niliendelea kusoma, nikafanya vizuri mitihani na nikafaulu.

"Ila ule mtihani niliokuwa ninapaswa kufanya wa online ambao ulikuwa ni wa muhimu sana, sikufanya kwa sababu nilikuwa natumia madawa (dawa za kulevya). Basi nilipewa zile pesa, mimi nikaenda kuvuta unga, yaani ninajutia hiyo nafasi mpaka leo, maana hiyo programu Tanzania nzima haikuwepo mpaka uende Uganda ule mtihani wa mwisho kabisa sikufanya maana kuna module 1 mpaka 4.

"Mzee alinipa pesa zote, alikuwa hana shida kabisa, nilimdanganya nimelipia kumbe mimi nimevuta unga, basi nilipomaliza chuo nikaenda kukaa nyumbani, mzee wangu. 

Itaendelea chapisho lijalo hapa DIRAMAKINI BLOG

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news