NA TITO MSELEM-WM
WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko ametatua mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika Kijiji cha Nayu Kata ya Dabalo wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma.

Inaelezwa kuwa, Kijiji cha Nayu kina jumla ya leseni 16 ambazo Mwekezaji ana leseni 8 na wanakijiji wana leseni 8 ambazo zinamilikiwa kihalali kwa kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Serikali.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo wa madini, Dkt. Biteko amesema, Wizara ya Madini inatoa leseni za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali, pale inapotokea leseni ipo ndani ya Hifadhi za Misitu ni lazima mmliki apate kibali kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TSF).

Aidha, Dkt. Biteko amemtaka Mwekezaji wa madini ya dhahabu katika kijiji hicho Sarehe Mohamed kujenga mahusiano mazuri na wanakijiji aliowakuta katika eneo hilo ili afanye kazi kwa ushirikiano.


Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Gift Msuya pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma Chagwa Marwa kufungua Soko la Madini katika kijiji cha Nayu ili kuwarahisishia wachimbaji wadogo mahali pa kuuzia madini yao na kusaidia kijiji kupata tozo kutoka kwenye madini yaliyopo kwene eneo lao.

Naye, Mbunge wa Chamwino ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora Deogratius Ndejembi amempongeza Waziri wa Madini kwa kukubali kuongozana naye ili kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.