Dkt.Biteko awasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti, asema kuna nuru kupitia soko la dhahabu

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Madini,Dkt.Doto Biteko amesema, changamoto ya vita kati ya Urusi na Ukraine inaweza kusababisha mahitaji makubwa ya madini ya dhahabu duniani.
"Uchumi wa madini nchini kwa kiasi kikubwa unatokana na madini ya dhahabu, ambayo huchangia takribani asilimia 80 ya mapato yatokanayo na rasilimali madini.

"Wachambuzi wa masuala ya uchumi duniani walitarajia bei ya dhahabu kuendelea kuwa tulivu kwa mwaka 2022, hata hivyo, bei ya madini ya dhahabu imepanda kutoka wastani wa dola za Marekani 1,412.98 Julai 2019 hadi kufikia 1,947.83 Machi, 2022

"Kuongezeka kwa bei ya dhahabu kunatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwepo wa UVIKO-19, vita kati ya Urusi na Ukraine inaweza kusababisha mahitaji makubwa ya madini ya dhahabu, hii ni kwa sababu watu na taasisi duniani hupendelea kuhifadhi thamani ya fedha zao katika madini ya dhahabu kwa kuwa ni amana iliyo salama zaidi hasa wakati wa mitikisiko ya kiuchumi"

"Kwa upande mwingine, ukuaji wa teknolojia umesababisha ongezeko la mahitaji ya madini ya palladium, nickel, aluminium, cobalt na madini ya kinywe (graphite), hivyo, bei ya madini hayo inatarajiwa kupanda na kuongeza fursa za uwekezaji;

Ameyasema hayo leo Aprili 29,2022 Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 leo bungeni jijini Dodoma.

Dkt.Biteko amesema, ili wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyopangwa,analiomba Bunge liridhie na kupitisha makadirio ya shilingi bilioni 83,445,260,000.0 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

GST

“Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutoa huduma, GST inakusudia kuboresha mifumo ya uchakataji, uhifadhi na usambazaji wa taarifa za jiosayansi kuhusu upatikanaji wa madini, kuwawezesha watumishi kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu.

"Pia kuboresha mazingira ya utendaji kazi na maslahi ya watumishi, kutangaza bidhaa na huduma zitolewazo na GST na kukamilisha kufanya mapitio na maboresho ya muundo wa taasisi ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya GST,”amesema Dkt.Biteko.

Pia amesema, katika kukabiliana na majanga ya asili ya jiolojia kama vile matetemeko ya ardhi, maporomoko ya ardhi, na milipuko ya volkano, GST inakusudia kukusanya takwimu kutoka vituo vitano vya kudumu vya kupimia matetemeko ya ardhi vilivyopo Arusha, Dodoma, Geita, Mtwara na Mbeya.

Dkt.Biteko amesema, lengo ni ili kujua matukio mbalimbali ya mitetemo, kuchakata takwimu zilizokusanywa kutoka katika vituo hivyo na kuhuisha ramani inayoonesha vitovu vya matetemeko ya ardhi nchini.

Tume

Amesema, Tume ya Madini itaendelea kuzihusisha mamlaka nyingine za Serikali zinazofungamana na sekta katika utekelezaji wa majukumu ikiwa ni pamoja na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Wengine ni Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA),taasisi za fedha, pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha changamoto mbalimbali zikiwemo za kisheria, mitaji, upatikanaji wa vibali, tozo na kodi ambazo zimekuwa zikiwakabili wachimbaji nchini zinatatuliwa kwa wakati na kwa maridhiano.

Pia amesema, Tume ya Madini itaendelea kuimarisha utendaji kazi wake kwa lengo la kuisimamia ipasavyo Sekta ya Madini nchini kwa kuboresha mazingira na vitendea kazi na kuwaongezea ujuzi na weledi.

TGC

Amesema katika kuhamasisha na kuhakikisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini zinaimarika, Serikali imeendelea kukiimarisha Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwa kuongeza fedha katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kununua vifaa vya kujifunzia.

Dkt.Biteko amesema, kituo hicho kinatoa mafunzo ya uongezaji thamani madini ikiwemo utambuzi, ukataji, uchongaji, ung’arishaji madini ya vito na utengenezaji wa bidhaa za usonara katika ngazi ya Astashada na Stashahada.
Amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa vijana wengi wanapata ujuzi katika nyanja hizo na kuwaongezea fursa za kupata ajira au kujiajiri.

“Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia STAMICO imejenga na kusimika miundombinu na mtambo wa kuzalisha makaa ya mawe kwa matumizi ya nyumbani katika eneo la TIRDO jijini Dar es Salaam. Uzalishaji wa majaribio ulifanyika kwa ufanisi. Aidha, shirika limeagiza mitambo miwili,”amesema.

Biashara yaimarika

Dkt.Biteko amefafanua kuwa, biashara ya madini nchini imeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi 2022 jumla ya kilogramu 39,682.94 za dhahabu, kilogramu 7,102.96 za fedha, karati 155,117.10 za almasi.

Pia kilogramu 15,377.44 za Tanzanite ghafi, kilogramu 130,582.28 za Tanzanite za ubora wa chini, karati 81,305.42 za Tanzanite iliyokatwa na kusanifiwa, tani 19,355.13 za madini ya shaba na tani 322.49 za madini ya bati zilizalishwa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news