Fainali ya Mkenda CUP 2022 ni kama 'Kariakoo Derby'

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Elimu, Sayansi ya Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro, Prof. Adolf Mkenda ameshuhudia mechi ya Fainali ya Kombe la Rombo yaliyojulikana kama Mkenda Cup 2022, ambapo timu ya Motamburu Kitendeni iliibuka na ushindi.
Katika mechi ya fainali iliyochezwa Aprili 24,2022 ilizikutanisha timu mbili za Motamburu Kitendeni na Ubetu Kahe, ambazo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 hadi dakika ya 90 na kwenda kwenye mikwaju ya penalti ambayo iliipa ushindi Motamburu Kitendeni kwa kushinda penalti 6 kwa 5 dhidi ya mpinzani wake.
Mshindi wa kwanza katika mchezo wa fainali ya Mkenda Cup 2022 aliibuka na kitita cha Shilingi milioni mbili pamoja na kombe, mshindi wa pili akiibuka na sh.milioni moja huku mshindi wa tatu ambayo ni timu ya Nanjara ikiibuka na sh.500,000 ambapo mfungaji bora aliondoka na kiatu cha dhahabu huku kipa bora akijishindia jezi, gloves na soksi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi hao, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.David Silinde ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye fainali ya mashindano hayo alipongeza washiriki wa mashindano hayo kwa vipaji vikubwa walivyovionesha huku akieleza jukumu lililobaki kuwa ni la Serikali kuendeleza vipaji hivyo.

Alisema mpango wa Serikali ni kujenga shule za vipaji kwenye kanda nane nchini ambazo zitasaidia kuibua vipaji ambapo kwa kupitia mashindano kama ya Mkenda Cup yatairahisishia Serikali kutambua vipaji vilivyopo kwa urahisi.

“Nimpongeze Mbunge wa Rombo, Prof. Mkenda ambaye ndiye mdhamini wa mashindano haya, kazi aliyoifanya kuunganisha vijana kwa timu 63 kwa zaidi ya miezi minne siyo rahisi, na vijana hawajamuangusha wameonesha kuwa Rombo kuna vipaji vikubwa na wapo imara,” alisema Mhe. Silinde.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rombo, Mhe. Prof. Mkenda alisema ataendelea kudhamini ligi hiyo ya mpira wa miguu kwa mwaka 2023 ambapo kwa sasa wataendelea kucheza mechi za kirafiki kwa kila Kata ambazo kila mchezo utakuwa na zawadi.
“Baada ya fainali hii tutaanza kucheza michezo ya kirafiki mpaka mwezi Desemba ambayo itaitwa Samia Friendship Tournament kwa heshima ya Rais wetu na kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya kwa Jimbo la Rombo,” alisema Prof. Mkenda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news