Biashara United Veteran yawachapa Musoma Veteran 3-1 Miaka 58 ya Muungano

NA FRESHA KINASA

TIMU ya Biashara United Veteran imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu ya Musoma Veteran katika mchezo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Mjini Musoma ikiwa ni Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ambapo Bonanza la michezo ya mpira wa miguu limefanyika likijumuisha timu nne ikiwemo timu ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Timu ya Chuo Cha Uuguzi Musoma, Biashara United Mara Veteran na Musoma Veteran likiratibiwa na Kituo cha Radio cha Victoria FM kilichopo Musoma.

Kabla ya mchezo huo wa fainali, ulichezwa mchezo wa kusaka mshindi wa tatu baina ya timu ya Chuo cha Uuguzi cha Musoma na timu ya Maendeleo ya Jamii Buhare. Ambapo timu ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare iliibuka kidedea kwa kushinda mikwaju ya penati 4-3.
Mratibu wa bonanza hilo Shomari Binda amesema, bonanza hilo limewezesha kuimarisha uhusiano mema, kuimarisha afya, kudumisha udugu na kuenzi mema yote yaliyofanywa na waasissi wa Muungano huo Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Aidha, Binda amewaomba Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na kushirikiana na serikali katika kuhakikisha Taifa linapiga hatua mbele za kimaendeleo.
Pia, Binda amewashauri vijana kujiepusha na vitendo viovu badala yake washiriki kikamilifu kutumia fursa mbalimbali na rasilimali zinazowazunguka kujipatia kipato halali sambamba na kushiriki michezo kujenga afya kwa manufaa yao.

Post a Comment

0 Comments