KMC FC yazuru kaburi la hayati Dkt.Magufuli kabla ya jambo lao Jumamosi

NA DIRAMAKINI

WACHEZAJI, viongozi pamoja na benchi la ufundi la timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC) leo wamezuru katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,hayati Dokta John Joseph Pombe Magufuli nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita.
Hiyo ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuenzi mchango wake katika sekta ya michezo alioufanya enzi ya uhai wake.Hayo yamebainishwa leo Aprili 21, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Mawasiliano wa KMC FC akiwa Chato mkoani Geita, Bi.Christina Mwagala.

KMC FC ambayo imeweka kambi wilayani Chato tangu Aprili 18, mwaka huu ikiwa ni mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar,uliopigwa Aprili 17,mwaka huu katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, inaendelea kutambua mchango mkubwa ambao hayati Dkt.Magufuli aliouonesha kwenye sekta hiyo enzi ya uhai wake.
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, ikiwa Chato imefika pia ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi na kupata mapokezi mazuri pamoja na ushirikiano mkubwa ikiwa ni pamoja na kufanikisha kufika nyumbani kwa hayati Dkt.Magufuli, lakini pia kutumia uwanja wa Magufuli unaomilikiwa na wilaya hiyo kwa ajii ya kufanya mazoezi.

“ KMC tunatambua mchango mkubwa ambao hayati Dkt.Magufuli aliufanya enzi ya uhai wake katika sekta hii ya michezo, hivyo ndio mana tukaona wakati huu ambao timu ipo huku Kanda ya Ziwa tufike nyumbani kwake kuzuru pamoja na kusalimia familia yake, lakini pia kufika kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi ambapo kimsingi tumepata mapokezi makubwa na tunawashukuru kwa hilo.

"Lakini pia wakazi wa Chato wameonesha kufurahishwa na uwepo kwa KMC, kwani wakati wa mazoezi wamejitokeza kwa wingi kuwasapoti wachezaji na hii kwetu kama timu tumechukua kama sehemu ya kutambua mchango wao kwetu na hivyo kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa pindi tutakapokuja huku kwa mara nyingine,"amesema.
Hata hivyo, KMC FC inaendelea kujiimarisha kuelekea katika mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania dhidi ya Geita utakaopigwa siku ya Jumamosi ya Aprili 23,mwaka huu katika Uwanja wa Magogo saa 16:00 jioni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news