Madiwani wawili Tanga Jiji wasimamishwa kwa kuonesha dharau kwa Naibu Meya

NA DIRAMAKINI

BARAZA la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga mkoani Tanga limeridhia kisimamishwa kwa madiwani wawili baada ya kuhusishwa na vitendo vya kumdharau Naibu Meya wa halmashauri ya jiji hilo, Joseph Colvas.

Ni kwenye kikao cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 kilichoongozwa na Naibu Meya wa jiji hilo, Joseph Colvas.

Madiwani waliosimamishwa ni Habiba Namalecha ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu na Swalehe Mwagilo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kirare.

Madiwani hao wamesimamishwa hadi mwezi April 2023 ambapo hawatohudhuria katika vikao vitatu vya mabaraza pamoja na kukosa stahiki zao.
Akitoa taarifa hiyo katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022 kilichofanyika jijini Tanga Mstahiki Meya wa halmashauri ya Jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloo mara baada ya baraza kugeuka kamati kwajili ya kujadili maswala ya kinidhamu amesema, wamechukua hatua hiyo ili madiwani hao kuwa mfano kwa madiwani wengine ambao wanakosa nidhamu kwa viongozi wao.

Meya Shiloo amesema kuwa, madiwani hao hawatahudhuria vikao vitatu vya kanuni pamoja na kukosa stahiki zao ambapo watatakiwa kurejea kwenye baraza hilo kwenye kikao cha mwezi wa nne 2023.

"Wajumbe 22 kati ya 28 waliohudhuria kikao hicho walimshauri Mstahiki Meya kuchukua adhabu dhidi ya madiwani hao ili iwe fundisho kwa madiwani tunaobaki na kulifanya Baraza letu liwe lenye nidhamu na kuleta maslahi kwa wananchi,"amesema Shiloo.

Meya Shiloo amesema kuwa, kutokana na kanuni za baraza hilo madiwani hao hawatahudhuria vikao vitatu vya mwezi wa saba, wa kumi na wa kwanza pamoja na vikao vingine vinavyohusiana na kamati vya kuandaa mabaraza hayo.

Hata hivyo, Mstahiki Meya Shiloo aliwataka madiwani hao kuheshimu mamlaka na sheria zilizopo katika kuongoza baraza hilo pamoja na sehemu nyingine ili kuweza kutatua changamoto zilizopo kuwa maslahi mapana ya wananchi.

"Nataka mamlaka yangu mliyonikabidhi nyinyi nyinyi wenyewe na ya naibu wangu myaheshimu wote na muyatii na Mamlaka ya yeyote yule atakayepewa dhamana ya kuliendesha baraza hili, haina maana Meya asipokuwepo baraza lisiendeshwe hilo halikubaliki,"alisema Meya Shiloo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja mstaafu Hamis Mkoba amewataka madiwani na watumishi wa halmashauri kuheshimu mamlaka ili kuepukana na migogoro inayoweza kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

"Madiwani mnatakiwa kwanza mnatakiwa muwe kitu kimoja na hamuwezi kuwa kitu kimoja kama hamuheshimiani, "amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news