Vijana waneemeka kupitia utekelezaji wa Anwani za Makazi nchini

NA IMMACULATE MAKILIKA-MAELEZO

MFUMO wa Anwani za Makazi nchini unatajwa kuwa na fursa lukuki kwa vijana ikiwa ni pamoja na kubuni na kushiriki kutengeneza miundombinu kwa ajili ya mfumo huo nchini.
Vijana wa Kampuni ya Photosilver inayotengeneza vibao vya Anwani za Makazi iliyopo mkoani Rukwa wakiendelea na utengenezaji wa vibao hivyo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi, Kundo Mathew ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi mkoani humo.(Picha na Jumaa Wange).

Akizungumza leo mkoani Rukwa wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi, Kundo Mathew alisema kuwa Serikali imeendelea kutimiza dhamira yake ya kutoa fursa mbalimbali kwa Watanzania, ambapo kupitia Mfumo wa Anwani za Makazi, vijana wenye ubunifu wamepata fursa ya kushiriki kutengeneza miundombinu kwa ajili ya Anwani za Makazi katika maeneo yao.

Akitolea mfano mkoani Rukwa, Naibu Waziri huyo alisema “Nakupongeza sana Mkuu wa Mkoa kwa kushirikisha vijana hawa wazawa wa mkoa huu katika kazi hizi za kubuni na kutengeneza namba na vibao vinavyotumika katika zoezi hili ni dhahiri kuwa watapata kipato kwa utaalamu wao na wanafanyakazi hii kwa kufuata vigezo vinavyotakiwa”

Sambamba na hilo Naibu Waziri Kundo, ameupongeza mkoa huo kwa utekelezaji wa Anwani za Makazi ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kazi ya kukusanya taarifa na kuingiza katika mfumo pamoja na kubandika vibao vya namba za nyumba na nguzo za barabarani.


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi, Kundo Mathew akionesha vibao vya Anwani ya Makazi wakati alipotembelea Kampuni ya Photosilver inayotengeneza vibao hivyo iliyopo mkoani Rukwa. Kulia ni Mmiliki wa Kampuni hiyo Imani Badeleya.


Alisisitiza “Hadi jana Aprili 26, 2022 mkoa huu umetekeleza kazi hii ya kukusanya taarifa kwa wastani wa asilimia 97.81 ikiwa ni nafasi ya 24 kati ya mikoa 31 ya Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, halmashauri zote zimetekeleza kazi hii kwa zaidi ya asilimia 90 zikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yenye asilimia 102.73 ikifuatiwa na Halmashauri ya Nkasi yenye asilimia 97.45 na Halmashauri ya Kalambo yenye asilimia 97.23”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Joseph Mkirikiti alisema kuwa mkoa wake umejipanga kukamilisha utekelezaji wa Anwani za Makazi ndani ya kipindi kilichopangwa.

Naye, Mmiliki wa Kampuni ya Photosilver inayotengeneza namba na vibao na, Imani Badeleya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa mbalimbali kwa vijana nchini.

“Tunakushukuru wewe Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuja kututembelea hapa katika karakana yetu, lakini pia tunaipongeza Serikali na mkoa wetu kwa kuendelea kutuamini sisi vijana na kutupa fursa kama hizi ambazo zinatusaidia kujiingizia kipato pamoja na kutumia ubunifu wetu katika kuchangia kuleta maendeleo ya mkoa wetu.” Alisema Badeleya.

Operesheni Anwani za Makazi inayoendelea kutekelezwa nchini kote ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Februari 8, 2022, ambapo alielekeza utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ufanyike kwa Operesheni na ukamilike ifikapo Mei, 2022 chini ya Uratibu wa Wakuu wa Mikoa.

Aidha, msingi wa kutekeleza mfumo huo ni ahadi iliyotolewa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) inayoelekeza wananchi wote kuwa na Anwani za Makazi ifikapo mwaka 2025. Vilevile ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na makubaliano Kikanda na Kimataifa kupitia Taasisi za Umoja wa Posta Duniani na Umoja wa Posta Afrika ambapo Tanzania ni mwanachama.

Post a Comment

1 Comments

  1. It is extremely good to hear and see.

    ReplyDelete