Mavunde awasilisha vipaumbele vitano vya wizara mbele ya FAO

NA DIRAMAKINI

NAIBU Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewasilisha vipaumbele vitano vya wizara mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bw. Qu Dongyu.
Vipaumbele hivyo ameviwasilisha leo Aprili 13, 2022 wakati wa kikao cha 32 cha Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) upande wa Afrika kinachoendelea jijini Malabo,Equatorial Guinea.

Katika kikao na Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dongyu, Mheshimiwa Mavunde amewasilisha vipaumbele ambavyo vinalenga kuifikia Agenda 10/30 na kutaka kuendelea kuimarisha ushirikiano na FAO katika kufikia malengo hayo.

Mheshimiwa Mavunde ameangazia upande wa kukuza uwezo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kutimiza malengo yake ya utafiti na uvumbuzi wa mbegu bora na kanuni bora za kilimo ili kuwawezesha wakulima wa Tanzani kulima kwa tija.
Kipaumbele kingine, Mheshimiwa Mavunde ameangazia upande wa uzalishaji mkubwa wa mbegu bora kupitia Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) na sekta binafsi kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kuagiza mbegu nje ya nchi, badala yake kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mbegu zinazitosheleza mahitaji ya nchi na kuuzwa nje ya nchi.

Pia Mheshimiwa Mavunde ameangazia uwekezaji kwenye Kilimo cha Umwagiliaji ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua ambacho kimekuwa kikiathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi.

Sambamba na kuimarisha huduma za ugani kwa kuwezesha mafunzo maalum ya zao moja moja ili kuongeza umahiri wa maafisa ugani katika kuwahudumia wakulima na kuwasaidia kulima kwa tija.

Kipaumbele kingine ni mpango wa ushirikishwaji wa vijana katika kilimo kupitia mfumo wa mashamba makubwa ya pamoja (block farms).

Post a Comment

0 Comments