Mbunge Aida Khenan ashiriki chakula cha pamoja na wafungwa

NA DIRAMAKINI

MBUNGE wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Aida Khenan (CHADEMA) amekula sikukuu ya Pasaka pamoja na wafungwa wa gereza la Kitete wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Akizungumza na Wafungwa wa gereza hilo alisema kuwa yeye kama mbunge alionelea pasaka hii ale pamoja na Wafungwa kwani na wao ni sehemu ya Watu wanaohitaji faraja katika kipindi kama hicho cha sikuukuu.

Pia aliwataka Wafungwa katika kipindi chote wawapo gerezani wajaribu kubadilika kama wanavyoelekezwa na askari ili kuwa raia bora na kujutia kile kilichowapeleka gerezani ili wasije wakakirudia.

Mbunge Khenan alidai kuwa, amefurahishwa na taarifa ya mkuu wa gereza hilo juu ya Wafungwa wote kupewa ujuzi mbalimbali ikiwemo kilimo bora,ufugaji sambamba na ujuzi mbalimbali na kuwataka kuutumia ujuzi huo katika kuendesha maisha uraiani baada ya kumaliza vifungo vyao gerezani.

“ujuzi mnaoupata hapa gerezani ni moja kati ya nyenzo muhimu kama itaenda kutumika vyema baada ya kumaliza vifungo vyenu italeta faraja hata kwa jamii baada ya kutoka gerezani,’’alisema.

Alisema, wao kuwapo gerezani isiwe sababu ya wao kukata tamaa bali ni muda wa wao kujitafakari na kumrudia Mungu wao ikiwa na kuona kuwa ni sehemu ya mapito katika maisha na kutengeneza mazingira mazuri ya kuwa raia wema na kuweza kukubalika katika jamii.
Awali mkuu wa gereza hilo la Kitete, SP Nichodemus Tenga alidai kuwa gereza lake limekuwa likiwapatia ujuzi wa namna mbalimbali Wafungwa likiwemo la kilimo bora na cha kisasa chenye kuleta tija na kuwa kutokana na hilo gereza hilo limeweza kuzalisha magunia 1,6000 za mahindi katika msimu uliopita wa kilimo na kuwa katika msimu huu wa kilimo wanatarajia kuvuna magunia 2000 za mahindi.

Alisema magereza lina nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwa jamii kwa kuzalisha mazao yote ya kimkakati na kuweza kuyaingiza sokoni na kuweza kutatua changamoto ya kupanda kwa bei mbalimbali ya bidhaa na kuondoa kero kwa jamii ya kupandisha bei kwa sababu wao watauza kwa bei elekezi ya serikali.

Mkuu huyo wa gereza alifafanua kuwa sasa hivi taifa lina uhaba wa mafuta ya kula na kuwa kama Magereza yatajengewa uwezo wa vifaa wanao uwezo mkubwa wa kuzalisha alizeti kwa wingi na tatizo hilo litakatoweka kabisa nchini kwa maana maeneo ya kulima waliyonayo ni makubwa na yanawezesha kuweza kutimiza ndoto hizo.

Wafungwa kwa upande wao walimuahidi mbunge kuwa, wao sasa wamebadili tabia zao na sasa ni watu wema na kuwa hata wakirudi uraiani watakuwa ni Walimu wa wenzao katika kutenda mema ikiwa ni pamoja na ujuzi walioupata kuutumia katika kujipatia kipato chao cha kila siku.

Mbunge aliweza kununua ng’ombe mmoja na mchele na kuwapatia sabuni za kuogea na kuweza kusherehekea sikukuu hiyo ya Pasaka

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news