Mwalimu Meijo Laizer:Rais Samia ametuheshimisha sana kupitia Royal Tour

NA GODFREY NNKO

MCHAMBUZI wa Masuala ya Siasa na Masuala ya Kijamii nchini, Mwalimu Meijo Laizer kutoka Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewaheshimisha kwa kiwango cha hali ya juu Watanzania kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imeionesha Dunia, Tanzania ilivyobarikiwa na vivutio mbalimbali vya utalii.
Pia Mchambuzi Mwalimu Laizer amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
 
"Awali ya yote nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kupitia Royal Tour ametuheshimisha sana duniani, Royal Tour imetujengea heshima kubwa kama Taifa na hakika huu ni ubunifu mkubwa na uzalendo mkubwa kwa Taifa lako, hongera sana Mheshimiwa Rais Samia;

Mwalimu Meijo Laizer ameyasema hayo kupitia mazungumzo na DIRAMAKINI BLOG wakati akielezea nguvu ya Royal Tour katika kuipaisha Sekta ya Utalii nchini Tanzania ikiwemo kuitangaza Tanzania katika uso wa Dunia.

Aprili 18, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza Uzinduzi wa Filamu Maalum ya Watanzania ya Royal Tour ambayo ni mahususi kwa ajili ya kutangaza utalii na uwekezaji wa Tanzania Kimataifa ambao ulifanyika jijini New York, Marekani.

Uzinduzi wa pili ulifanyika Aprili 21, 2022 katika jiji la Los Angeles nchini Marekani na hivi karibuni ratiba itaendelea hapa nchini.

"Kwa hiyo ni ni dhahiri nchi yetu imejulikana katika uso wa Dunia kwa ubunifu mkubwa wa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Juzi usiku nilipata muda mrefu wa kutafakari ubunifu huu mkubwa katika nyanja mbalimbali.

"Mosi, ubunifu mkubwa wa Rais wetu nimeona katika suala la ujenzi wa Madarasa ya UVIKO-19 kwa nchi nzima, jambo hili limekuwa 'surprise' kubwa kwa Watanzania.

"Wazalendo wa nchi hii wamefurahia sana kwa ubunifu huu mkubwa wa Rais, kwani imeonesha Serikali ya Awamu ya Sita inajali wananchi wake,"anasema Mwalimu Laizer.

Anasema, hayo ni mambo mazuri na makubwa japo wapo wenye chuki binafsi na Mheshimiwa Rais Samia ambao walifika mahali wakata kuhoji utekelezaji wa miradi hiyo ya UVIKO-19.

Jambo la pili katika ubunifu mkubwa, Mwalimu Laizer anasema kuwa, Rais Samia amefanikisha kujenga umoja, uhuru wa kutoa maoni na mshikamano ndani ya nchi.

Sambamba na kutengeneza mazingira mazuri na salama kwa Watanzania katika kushiriki masulaa ya kisiasa kwa dhana ya uimarishaji wa demokrasia kwa vyama vya siasa nchini.

"jambo la tau ni funga kazi ya ubunifu mkubwa wa Royal Tour ambayo imekuwa gumzo kubwa duniani, Wazungu wanaulizana hii nchi ilyojaa kila rasilimali vitu, ipo katika Dunia ipi?

"Duniani wanajiuliza inakuaje Mlima Kilimanjaro umekua sehemu ya Tanzania na Afrika? Kwa nini haijawa Bara la Ulaya, Bara la Amerika au Bara la Asia? Kwa nini iwe Afrika na kwa nini iwe Tanzania? Wanajiuliza inakuwaje twiga, tembo, chui na simba wanapatikana nchini Tanzania na siyo Uingereza, siyo Ujerumani, siyo Norway, siyo Japan,na siyo Ukraine na wala siyo Russia?

"Inakuwaje Tanzania imekuwa sehemu ya Bara la Afrika na isiwe katika Bara la Amerika au Bara la Ulaya? Wazungu wanapita katika wakati mgumu wa kufanya utafiti wa kina juu ya Taifa letu kwa namna Mwenyenzi Mungu alivyotujalia rasilimali nyingi, kubwa na nzuri katika uso wa nchi yetu na uso wa Dunia, sote tuna kila sababu ya kumtukuza Mungu kwa kutupatia Taifa zuri kama hili,"anafafanua kwa kina mchambuzi huyo mbobezi katika masuala ya kisiasa na kijamii, Mwalimu Laizer.

Katika hatua nyingine, Mwalimu Laizer anasema, sisi kama nchi tuna kila sababu ya kumpatia kongole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake mkubwa ambao umelifanya Taifa letu kujulikana duniani kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi yetu.

"Ni dhahiri kabisa wapo Watanzania wanajiuliza kwa nini suala la Royal TOUR limetokea katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan? Inakuwaje kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na Awamu ya Tano jambo hili halijafanyika, inakuwaje leo katika Serikali ya Awamu ya Sita?

"Mzee ruksa Rais ya Awamu ya Pili, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi amewahi kusema kila zama na kitabu chake, hivyo kwa jambo hili la Rais wetu Samia Suluhu Hassan kubuni njia bora ya kuitangaza nchi yetu imeweza kufanya Serikali ya Awamu ya Sita kuandika KITABU CHAKE kilichojaa dhamira njema ya kutaka kujenga Uchumi wa Taifa Letu,"amesema Mwalimu Laizer.

Amesema, kupitia Royal Tour, inakwenda kuiwezesha Tanzania kujijenga katika mambo makuu ikiwemo kutengeneza Uchumi Mkubwa kwa Nchi kama ilivyobainishwa katika Ilani ya CCM 2020-2025.

Pia kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni kwa lengo la kuimarisha uchumi kwa Taifa, kujenga heshima ya Taifa katika uso wa Dunia,kujenga uimara na wigo wa kuzungumza lugha ya Kiswahili kwa wageni au kwa watalii wanaotazamia kutembelea nchi yetu.
Mambo mengine, Mwalimu Laizer amesema ni kuongeza ajira kwa vijana wa Taifa letu,kufanya nchi yetu kurejea katika Uchumi wa Kati, kuongeza na kuimarisha Diplomasia ya Kimataifa kama Ilani ya CCM inavyoelekeza.

"KONGOLE Mama Yetu, KONGOLE Rais Wetu,KONGOLE Mzalendo Wetu.Ni dhahiri kwa kazi hii kubwa inayofanywa na Rais wetu kila Mtanzania ana kila sababu ya kumuunga mkono Kiongozi Wetu Mkuu bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kwani jitihada hizi zinajenga Uchumi Imara kwa Taifa Letu na Si vinginevyo,"ameeleza Mwalimu Laizer.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news