NMB yakusanya Bilioni 74.3/- kupitia Hati Fungani (NMB Jasiri)

NA DIRAMAKINI

BENKI ya NMB imefunga mauzo ya Hati Fungani ya Jasiri (NMB Jasiri Bond) kwa mafanikio makubwa iliyoweka rekodi ya makusanyo Afrika Mashariki na Kati ya Shilingi Bilioni 74.27 na kuvuka lengo la Shilingi Bilioni 25, ufungaji ulioenda sambamba na kuiorodhesha rasmi hati hiyo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Naibu Katibu Mkuu - Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, akigonga kengele kama ishara ya kuorodheshwa rasmi 'NMB Jasiri' kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni; Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) - Moremi Marwa(kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB - Ruth Zaipuna na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama (kulia).

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu - Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, ametangaza rasmi kuorodhozeshwa kwa hati fungani ya Jasiri na sasa kuanza kununuliwa na kuuzwa kupitia soko la hisa la Dar es salaam.

Akizungumza Mafuru aliipongeza NMB kwa ubunifu chanya wa Jasiri Bond, hati fungani iliyolenga kukusanya fedha ili kutoa mikopo kwa biashara ndogo ndogo na za kati zinazo milikiwa au kuongozwa na wanawake na biashara ambazo bidhaa au huduma zake zinamgusa mwanamke moja kwa moja.

“Hii sio mara ya kwanza kwa NMB kuja na Hati Fungani na kuvuka lengo la makusanyo, hii ni mara ya nne na kwa hati hii ambayo ni ya kipekee, kama jina lake lilivyo, kumekuwa na ujasiri mkubwa sana, kwani jina Jasiri linaashiria mambo mengi sana.

“Ujasiri wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ya kuiruhusu Hati Fungani hii kuingia sokoni kabla hata ya sheria zake hazijawa tayari, jambo linalothibitisha imani ya mamlaka hii kwa NMB ilivyokuwa kubwa.

“Lakini pia, NMB ikalenga kupata Shilingi Bilioni 25 na hatimaye inafunga mauzo ikiwa imepata zaidi ya mara tatu ya lengo, hii ni kuthibitisha kwamba kuna nguvu kubwa ya kiuchumi miongoni mwa wanawake, tunachotakiwa ni kuweka mazingira wezeshi ya kuwaamini kama wenzetu NMB walivyofanya,” alisisitiza Mafuru.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema NMB ilipokea maombi 1,630 yaliyowezesha kukusanya Shilingi Bilioni 74.27 badala ya Bilioni 25 na kuwashukuru wateja na wawekezaji wote kwa kuiamini benki hio.

“Kuaminika kwa NMB katika hili kunathibitishwa na kuwa asilimia 96 ya waliotuma maombi ya kununua Hati Fungani, yamepitia katika matawi yetu, huku asilimia 4 tu yakifanyika kupitia Madalali wa Soko la Hisa waliosajiliwa”.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), Nicodemus Mkama, aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa NMB, kwa kufanikisha uuzwaji wa ‘Jasiri Bond’ kwa Umma wa Watanzania na hatimaye kufikia hatua ya kuiorodhesha DSE, tayari kwa mauzo ya walionunua na manunuzi ya waliokosa katika mchakato uliofungwa.
Naibu Katibu Mkuu - Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji - CPA Nicodemus D. Mkama, Mkurugenzi Mkuu wa DSE - Moremi Marwa, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB - Ruth Zaipuna, Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya NMB - Juma Kimori pamoja na wawakilishi kutoka FSD Africa, Ubalozi wa Uingereza, International Finance Co-operation (IFC), Orbit Securities Ltd na UN Women wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya kuorodhesha hati fungani ya NMB Jasiri katika Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE).

Wengine waliohudhuria hafla hii ni Mkurugenzi Mkuu WA DSE, Moremi Marwa, pamoja na wawakilishi kutoka FSD Africa, Ubalozi wa Uingereza, International Finance Co-operation (IFC), UN Women na Orbit Securities Ltd.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news