Polisi aliyefutwa kazi, kunusurika kifo kwa utumiaji dawa za kulevya alivyogeuka kuwa nuru kwa Waraibu Tanzania-5

NA GODFREY NNKO

CHAPISHO la Aprili 22, 2022 tuliona namna ambavyo, Bw.Twaha Amani ambaye alikuwa askari wa Jeshi la Polisi na baadaye mwalimu wa shule ya sekondari, ambapo kote huko alifukuzwa kazi kutokana na uvutaji na kujidunga dawa za kulevya ambazo zilimvurugia mfumo wote wa maisha yake alivyokimbia nyumba ya upataji nafuu, lakini baada ya kuona mambo ni magumu alirejea tena. Endelea...

Apata Mchumba akiwa Sober House

“Baada kama miaka mitatu nikataka kuondoka,mmiliki wa Sober akakataa, akaniomba nikae hapo na atanilipa na marupurupu jumla laki moja, nikaona ni pesa ndogo ila nikaendelea kufanya kazi, sasa wakati nipo Sober kulikuwa na dada jirani ambaye alikuwa analeta kuku tumchinjie, maana kwao walikuwa ni Waislamu.

"Lakini anafanya kazi za ndani kwa Wakristo, alikuwa analeta kuku nimchinjie maana kwao walikuwa ni Waislamu, nikajikuta tunaingia kwenye mahusiano, ambaye ni mke wangu sasa hivi na kwao ni Mwanga (Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro) ila alikuja kufanya kazi, basi tukiwa kwenye mahusiano bahati mbaya au nzuri nikampa mimba."

Uamuzi mgumu

"Na wakati huo nilikuwa nimeshatembea na wanawake wengi pale Bomang’ombe baada ya kuwa niko vizuri kiafya, sivuti tena unga, basi nikajifikiria tayari nina umri wa miaka 38 sijazaa mtoto wala sina mke basi nikaona huyu mwanamke ni wa kuoa na ukizingatia alikuwa na tabia nzuri amekulia mazingira ya dini.

"Basi nikatoa taarifa kwa bibi yangu, ndugu zangu, mama yangu na hata huyo mmliki wa Sober na mwaka huo ilikuwa 2019 mwishoni, basi ndugu zangu wakawa wameafiki kwamba nioe, sema huyo bosi wangu alionyesha kuniogopesha kama sitaweza kupanga chumba na maisha, basi nikatafuta chumba cha kupanga na nilikuwa na elfu sitini tu mfukoni na nina kitanda.

Mchumba ampiga tafu kifedha

"Yule dada naye alikuwa ana elfu themanini, akanipa ili ninunue vitu vya ndani, nikanunua mapazia na vitu vingine na wakati huo mimba inazidi kukuwa na hapo hawezi kufanya kazi tena na ilikuwa mwaka 2020 ikabidi aondoke aende kwao, lakini alipitia pale nilipopanga akapaona tukaongea akaondoka ila hakukaa sana kwao akarudi tukaendelea kuishi.

"Kwa hiyo mimi nikawa naenda Sober, ninarudi jioni kadri siku zilivyozidi kwenda ndipo mimba ilivyozidi kukuwa, karibu miezi tisa ikabidi nimpeleke kwao kwa ajili ya kujifungua na nyumbani nilikuwa nimeshatoa taarifa, siku zilifika akajifungua vizuri.
Bw.Twaha Amani akiwa na familia yake baada ya Mwenyenzi Mungu kumnusuru katika mapito magumu aliyopitia kwa miaka mingi kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya (heroine) kwa wingi ambazo zilisababisha kufutwa kazi ya uaskari, ualimu na sasa ameanza maisha mapya.

"Aliendelea kupata huduma ya uzazi huko kwao na ikawa anataka kutoka nje nikawapa taarifa nyumbani, wakasema asitoke nje afungiwe ndani ili umuoe kabisa, mfunge ndoa sisi tunachanga hela za harusi na zikafika milioni sita."

UVIKO-19 yakwamisha harusi yao

"Ilikuwa imebaki kama siku mbili tufunge ndoa, Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim akatangaza marufuku ya mikusanyiko maana kulikuwa na Corona ile ya kwanza na shule zilifungwa siku ile ile, basi sisi tukafanya mchakato tukafunga ndoa tu, tukaondoka zetu nyumbani Bomang'ombe,"anasema.

Tangazo hilo lilitolewa Machi 17,2020 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa akisema, “Mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, semina, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali za shule na shughuli nyingine za kijamii ambazo si muhimu.

“Lakini pia tumefunga shule zote za awali, msingi na sekondari hadi kidato cha sita na zitafungwa kwa siku 30 kuanzia leo Machi 17, 2020.Wizara itafanya marekebisho ya ratiba ya kidato cha sita ambao wanatarajiwa kufanya mitihani tarehe 4 mwezi wa Mei. 
 
"Watakuwa na muda mfupi kwa hiyo itasogezwa tena mbele kadiri ya matokeo yatakavyojitokeza ili nao wapate nafasi ya kusoma kwa kipindi kile kile kilichokubalika kwa mujibu wa ratiba hiyo,”Waziri Mkuu alinukuliwa wakati huo, ambapo tangazo hilo lilivuruga mipango ya harusi ya Bw. Twaha Amani.

Bw. Twaha Amani ambaye aliwahi kuwa askari wa Jeshi la Polisi akiwa anafanya kazi mkoani Tabora na baadaye kuwa mwalimu wa sekondari wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza ambapo kote huko alipoteza kazi kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya anasema,

"Wakati tukiendeleza maisha yetu maisha yalianza kuwa magumu, maana nipo na watu wawili wananitegemea ikabidi nianze mchakato wa hela, basi nikipata mtu anataka kuja pale Sober, mimi naongea nae vizuri kabla, kama ni laki tatu na nusu, bosi ninampa laki tatu na mimi ninabaki na changu kama elfu hamsini.

"Nilianza kuongea na bosi wangu ili aniongezee mshahara, kwani mambo ni magumu ninapaswa kupanga vyumba viwili ninunue gesi na chakula na mambo mengine na ukizingatia mtoto anazidi kukua. Kwa hiyo, laki moja ikawa ni ndogo sana kuendesha maisha yangu na bosi akawa ananiahidi kila siku kuniongezea bila manufaa.

Arejea Misungwi kama atafikiriwa

"Mwaka 2021 nikiwa hapo hapo Sober Bomang'ombe baada ya kuona majukumu yameshakuwa mengi mtoto anakuwa na chumba kimoja hakistahili tena,ikabidi nijaribu kwenda tena Mwanza katika Halmashauri ya Misungwi kwenda kufuatilia ajira yangu niliyoajiriwa mwaka 2012 ila baada ya kukutana na Afisa Elimu alinikutanisha na Afisa Utumishi.

"Nikaongea nae kwa kina na kumwambia matatizo ambayo niliyapitia alinisikiliza vizuri sana mpaka mwisho akaniambia...daaah pole sana."

Hakuna kazi tena

"Sasa ipo hivi, wakati Magufuli (hayati Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli) anaingia madarakani 2015 alifanya mabadiliko makubwa sana kwenye wafanyakazi hewa, mishahara hewa pamoja na vyeti feki kwa hiyo ni bora nianze ku-apply upya,basi baada ya kuniambia hivyo ikabidi nirudi zangu Moshi, kule Bomang'ombe Sober kwa kuwa huko ndipo nilikuwa nikifanya kazi na kupata riziki, huku nikiwa nimepanga chumba kimoja mimi na familia yangu,"amefafanua Bw.Amani.

ITAENDELEA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news